In Summary

• Polycarp Igathe atarajiwa kutangazwa mgombea ugavana Nairobi, naibu wake akiwa Tim Wanyonyi.

•  Baada ya mazungumzo, inaarifiwa Azimio-One Kenya walikubaliana Jubilee kutoa mgombea na ODM kutoa mgombea mwenza wa ugavana Nairobi.

Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga akiandamana na Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, Gavana wa Machakos Alfred Mutua, Gavana wa Kaunti ya Kitui Charity Ngilu miongoni mwa viongozi wengine wakati wa Azimio NDC mnamo Machi, 12, 2022./
Image: MERCY MUMO

Duru zinaarifu kwamba huenda chama cha Jubilee kikamuidhinisha aliyekuwa naibu gavana wa Nairobi Polycarp Igathe kuwa mgombea ugavana wa Nairobi na hivyo kuzua sintofahamu kuhusu uwezekano wa mfanyibiashara Richard Ngatia kuidhinishwa na chama hicho.

Taarifa zinasema kwamba muungano wa Azimio-One Kenya umekaribia kuafikia uamuzi wa kumkabidhi Polycarp Igathe bendera ya kuwania ugavana kwa niaba ya muungano huo huku naibu wake akitajwa kuwa mbunge wa sasa wa Westlands, Tim Wanyonyi ambaye pia alikuwa akilenga tiketi ya chama cha ODM kuwania ugavana Nairobi.

Ikiwa taarifa hizi ni za ukweli, basi itamaanisha ni mwisho wa barabara kwa mfanyibiashara Richard Ngatia ambaye alikuwa akilenga tiketi ya Jubilee kuwania ugavani katika jiji kuu huku wengi wakimshabikia na kumtaja pakubwa kwamba ndiye mwaniaji faafu zaidi wa kulikomboa jiji kutoka kwa mrundiko wa makosa ambayo mtangulizi wake Mike Sonko aliyafanya mpaka kupelekea kung’atuliwa kama gavana.

Inasemekana kwamba baada ya mazungumzo ya kina baina ya vyama tanzu vya muungano wa Azimio-One Kenya, uamuzi uliafikiwa kwamba chama cha Jubilee chake rais Kenyatta kipewe nafasi ya kutoa mgombea ugavana na kile cha ODM kikapewa nafasi ya kutoa mgombea mwenza ugavana Nairobi.

Jubilee kilikuwa na wawaniaji watatu ambao wote walikuwa wanalenga tiketi ya kuwa gavana. Watatu hao walikuwa ni gavana wa sasa Ann Kananu, mfanyibiashara Agnes Kagure na Richard Ngatia ambaye alikuwa ameanza kujizolea umaarufu kutokana na mabango yake mengi yaliyopakiwa katika pande nyingi tu za jiji la Nairobi.

View Comments