In Summary

• "Nitakapoapishwa kuwa gavana wako hapa Bukhungu, nitampa mtu yeyote atakayekuja na pikipiki KSh 1000" - Malala

Seneta wa Kakamega ambaye pia anawania uagavana, Cleophas Malala
Image: Facebook//CleoMalala

Mgombea ugavana kaunti ya Kakamega, Cleophas Malala kwa mara nyingine tena amezua maoni kinzani kwa ahadi zake zenye utata mkubwa kwa wakaazi wa kaunti hiyo yenye wapiga kura wengi katika mkoa wa Magharibi ya Kenya.

 Malala ambaye ni seneta wa sasa anayelenga kumrithi gavana Oparanya kama gavana alisikika hivi karibuni akiwaambia wahudumu wa bodaboda wote katika kaunti hiyo kwamba siku ya uchaguzi mkuu atamlipa kila mwenye pikipiki shilingi elfu moja taslimu za Kenya ambaye atampata kwenye kituo cha kupiga kura akimlindia kura zake ziziibwe.

“Siku hiyo, ikiwa wewe ni mwendesha bodaboda, usiende kazini baki katika kituo chako cha kupigia kura na ulinde kura zangu, na nitakapoapishwa kuwa gavana wako hapa Bukhungu, nitampa mtu yeyote atakayekuja na pikipiki KSh 1000. Hayo yatakuwa malipo yangu kwa kazi iliyofanywa vizuri,” Cleophas Malala aliahidi.

Malala ambaye anawania kutoka mrengo wa Kenya Kwanza alisisitiza msimamo wa mpeperusha bendera wao William Ruto kwa kusema kwamba kura zao hata moja haitaibwa na kuwataka wafuasi wao wote kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi huo unaotarajiwa wiki moja ijayo.

“Hakuna mtu atakayeiba kura zetu kwa sababu tutalinda kura zetu wakati wa uchaguzi. Tafadhali tupige kura kwa amani, na ninataka kuwaambia jamii zote hapa Kakamega kwamba wasiwe na wasiwasi kwani hatutadharau jamii yoyote,” alisema Jumapili, Julai 31, wakati wa mkutano wa Kenya Kwanza katika uwanja wa Bukhungu.

Hii si mara ya kwanza seneta huyo anatoa ahadi zenye utata ambazo wengi wanadai haziwe zikadumishwa kwani mapema mwaka huu alinukuliwa akisema kwamba pindi atakapochaguliwa ataweka bafu za maji moto katika kila boma kwenye kaunti ya Kakamega.

“Tuko na wazee, kina mama ambao hata hawawezi kuinama kwa bafu kuoga, unapata wameweka beseni maji kwa bafu, mama mzee hawezi inama kwa sababu magoti yao yameisha. Hawezi oga kama ameinama. Mimi nitafanya kitu rahisi sana, kwa sababu kama maji yamefika kwa nyumba yako, nitaweka ‘hot showers’ nataka watu wangu waoge kama wamesimama kwa sababu kuoga kama umesimama si jambo gumu,” alijipigia debe Malala

View Comments