In Summary

• Akizungumza katika hafla hiyo, Odinga alisema kwamba firimbi ni ya aina mbili moja ikiwa ile ya kufukuza wezi na wafisadi na ya pili alisema ni ya kurausha watualfajiri na mapema ili kumpigia kura.

Mgombea urais kwa tikiti ya vuguvugu la Azimio la Umoja One Kenya Raia Odinga Jumamosi katika ukumbi wa Kasarani alizindua vuguvugu la firimbi, kundi ambalo kazi yao itakuwa ni kutembea mitaani na firimbi midomoni wakiwarausha watu kutoka kupiga kura kwa wingi mnamo Agosti 9.

Akizungumza katika hafla hiyo, Odinga alisema kwamba firimbi ni ya aina mbili moja ikiwa ile ya kufukuza wezi na wafisadi, hapa akionekana kumlenga mpinzani wake William Ruto ambaye kwa muda mrefu amekuwa akipakwa tope la wizi na ufisadi. Firimbi ya pili alisema ni ya kurausha watualfajiri na mapema ili kumpigia kura.

“Vijana mpo, sasa leo tunataka leo tuzindue hiyo Rauka Operesheni Firimbi Movement. Firimbi iko mara mbili, iko moja ya ufukuza wezi na kumaliza ufisadi, na ile ya pii ni kufanya watu warauke mapema tarehe tisa saa kumi waende kwa vituo kupiga kura,” Raila alisema.

Mgombea huyo wa urais hakuachia hapo bali alizidi mbele na kuonesha mfano jinsi milio ya aina hizo mbili za firimbi itakavyofanywa ili kutofautisha ule wa kuamsha watu kuenda kupiga kura na ile ingine ya kufukuza mwizi.

Kwingineko mgombea urais wa UDA William Ruto naye akiwa Nyayo alizidi kurindima ngoma yake huku akisema kwamba uongozi wake tu ndio wenye ahadi za kikweli za kumaliza ufisadi humu nchini na kuwarai Wakenya wote kukumbatia mfumo wake amabo alisema unazingatia sana uchumi tofauti na ule wa washindani wake aliosema unazingatia sana katiba na vyeo.

Mikutano ya wawili hao ilifanyika sambamba katika viwanja hivyo tofauti ndani ya jiji la Nairobi ambapo ndio ilikuwa siku ya mwisho kufanya kampeni rasmi huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa kufanyika siku mbili zijazo.

Kinyang’anyiro cha kutafuta mrithi wa rais Uhuru Kenyatta kiliwavutia wagombea wengi ila tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC  ikawachuja wengi na kupunguza orodha hiyo wagombea wanne ambao ni Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya, William Ruto wa Kenya Kwanza, George Wajackoyah wa chama Cha Roots na David Mwaure wa chama cha Agano.

View Comments