In Summary

•Peter aliweka wazi kwamba tayari ameanza juhudi za kumtafuta mkewe jijini Nairobi kwa kutumia picha yake.

•Vivian alifunguka kuhusu tabia ya mumewe ya kuwa na wanawake wengi, jambo ambalo lilimfanya atoroke.

Gidi na Ghost Studioni
Image: RADIO JAMBO

Peter Sankale Kesier ,31, kutoka Narok alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Vivian Kwamboka ,25, ambaye alikosana naye mapema mwaka huu.

Peter alisema ndoa yake ya miaka 10 ilisambaratika mwezi wa sita wakati mkewe alipoenda jijini Nairobi kwa ajili ya kazi.

Alisema mkewe alienda na kumuachia watoto watatu baada ya kutafutiwa kazi na rafiki yake.

"Nilimuoa akiwa na umri wa miaka 16. Yeye alikuwa amefikisha umri wa kuolewa.Kuna rafiki yake alimtafutia kazi Nairobi. Tajiri wake alimtumia nauli, yeye akatoka bila mimi kujua. Hakunieleza. Nilikuta nyumba ikiwa imeng'ara, akaacha watoto. Tumekuwa tukizungumza, wakati mwingine roho yake inakuwa nyepesi, wakati mwingine anakuwa mgumu hata ananiblacklist. Kila kitu nilikuwa nashughulikia, ingawa ata yeye alikuwa na kazi yake hapa Narok. Aliamua kuenda tu ," Peter alisema.

Peter aliweka wazi kwamba tayari ameanza juhudi za kumtafuta mkewe jijini Nairobi kwa kutumia picha yake.

"Kama hatutapatana nimeamua nitafika huko Nairobi, hata nimeanza safari, niko Mwiki. Kuna rafiki yake ananitumia picha zake kwa Facebook. Nitatumia hizo picha zake kumtafuta. Nimebeba picha mfukoni nataka kuenda nikiulizia mwanadada kama huyo anapatikana wapi. Nataka nimtafute ama nijue ukweli. Mimi nimechoka," alisema.

Vivian alipopigiwa simu, Peter alitumia fursa hiyo kumuomba amwambie ukweli.

"Shida iko wapi. Niambie tu msimamo wako nijue ukweli. Niambie ukweli niache kusononeka. Niko karibu kufika Mwiki. Mahali unakaa ndo sijui.Kuja hapa steji tuende," Vivian alisema.

Vivian aliweka wazi kwamba ameskia ombi la mumewe na akaahidi kurudi nyumbani.

"Nimeskia, nitakuja nyumbani. Najua watoto wanateseka, lakini wewe hujui kama mimi nateseka. Unadhani niko na roho kama ya hizi mawe ziko hapa.Ukiwa na yeye kwa nyumba haoni kama wewe ni bibi. Lakini ukitoka ndo anaona wewe ni wa maana," Vivian alisema.

Aliendelea kufunguka kuhusu tabia ya mumewe ya kuwa na wanawake wengi, jambo ambalo lilimfanya atoroke.

"Kunipiga ata sio shida, hiyo mambo ya wanawake wengi ndiyo hufanya nitoke nikae pekee yangu. Alikuwa ameoa mwanamke mwingine nikakubali. Sasa ikawa anabadilisha leo analeta huyo, kesho analeta mwingine. Nilikuwa nimevumilia. Watu wote wananiambia nivumilie. Lakini hiyo kuvumilia akaona ni ujinga. Nilikuwa nimeenda akaanza kusema eti nilienda umalaya Nairobi. Mimi nikasema kama anasema hivyo acha nirudi," Vivian alisema.

Hata hivyo, alikubali kurudi kwa ndoa yake, ila akamsihi mumewe aache kuleta wanawake wengi nyumbani.

"Mimi nitarudi nyumbani. Mambo ya wanawake achana na wao. Huna mali ya kutosha ya kuoa wake wawili. Mimi hukwambia hakuna shida, kuoa wa pili utaoa, mimi sitakukataza. Nilikupatia nafasi ukaona Kenya yote ni yako," alisema.

Gidi hata hivyo alimshauri mwanadada huyo asikutane na Peter akiwa pekee yake.

Peter alimalizia kwa kumwambia mkewe, "Nakupenda zaidi. Hata leo niko Mwiki nikikutafuta. Nimelala kwa barabara nikikutafuta. Tafadhali rudi nakupenda. ."

Vivian kwa upande wake alimwambia, "Bado nakupenda kama mke wangu. Nakuomba nikirudi nyumbani tukae vile tulikuwa tunakaa. Uache mambo ya wanawake wengi. Usishinde ukionyesha watu picha yangu. Nitakutafuta. Mahali uko nitakupigia simu."

Je, ushauri ama maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?

View Comments