"Nimechoka sasa nataka bibi na watoto" Ericko asema

Mcheshi Eric Omondi amehakikishia mashabiki wake kuwa ataoa binti atakayeshinda msimu wa tatu wa onyesho la ‘Wife Material’

Muhtasari

•Omondi ambaye aliachana na aliyekuwa mpenzi wake Muitaliano , Chantal Grazioli mwaka wa 2019 baada ya kuchumbiana kwa miaka minne na nusu amesema kuwa wazo la kuanzisha onyesho la Wife Material lilitokana na nia yake ya kutafuta bibi ili aanzishe familia.

Mcheshi Eric Omondi
Mcheshi Eric Omondi
Image: Instagram

Mcheshi Eric Omondi amehakikishia mashabiki wake kuwa ataoa binti atakayeshinda msimu  wa tatu wa onyesho la ‘Wife Material’

Msanii huyo ametangaza kuwa amechoka kuishi bila mke na kusema kuwa anataka familia kuona kuwa miaka yake bado inasonga

Kupitia ukurasa wa Instagram, mcheshi huyo amesema kuwa atazindua awamu ya tatu ya onyesho la Wife Material ndani ya kipindi cha mwezi mmoja  ujao baada ya awamu ya pili kukatizwa kwa hali tatanishi mwezi uliopita hata kabla ya kuanza vizuri.

Omondi ambaye aliachana na aliyekuwa mpenzi wake Muitaliano , Chantal Grazioli mwaka wa 2019 baada ya kuchumbiana kwa miaka minne na nusu amesema kuwa wazo la kuanzisha onyesho la Wife Material lilitokana na nia yake ya kutafuta bibi ili aanzishe familia.

"Nyakati zingine huwa naketi najiuliza nia ya kuanzisha onyesho hili ilikuwa gani, kisha nakumbuka nia kuu. Nilikuwa natafuta bibi wa kuoa, nitulie nianzishe famlia ila mambo yakatendeka na hiyo ndiyo hali ya maisha" Ericko aliandika.

Onyesho la kwanza lilikatizwa baada ya mcheshi huyo kukamatwa baada ya amri ya mkurugenzi mtendaji wa bodi ya uainishaji wa Filamu nchini Kenya(KFCB), Ezekiel Mutua aliyedai kuwa Omondi alikuwa amekiuka masharti ya filamu na michezo ya jukwaani kwa kutengeza na kusambaza filamu za Wife Material. Msimu wa pili wa onyesho hilo haukufua dafu pia baada ya kile Omondi alisema ni kupotoka na kukosa kudhibitika kwa mgombeaji mmoja.

Hata hivyo, Omondi ameendelea kutangaza msimu wa tatu akihakikishia mashabiki, familia na marafiki kuwa mara hii ataoa atakayeshinda.

Nataka kuwahakikishia mashabiki , familia na marafiki wangu  kuwa nitaanzisha awamu ya tatu ya Wife Material hivi karibuni na itahusisha nchi za Ethiopia, Rwanda, South Sudan na Nigeria na nawahakikishia kuwa atakayeshinda msimu huu namuoa na nitulie naye, hili nimewaahidi. Hata mimi nimechoka nataka bibi na watoto, nataka familia.. nafikisha niaka 40 miezi tisa ijayo” Omondi aliandika.