Je, Omosh anahitaji usaidizi? Video inayomuonyesha akiwa mlevi chakari yaghadhabisha Wakenya

Wanamitandao wamependekeza mwigizaji huyo kupelekwa kwenye taasisi ya kurekebisha tabia

Muhtasari

•Madai yameibuka kuwa mwigizaji huyo alizama kwenye uraibu wa pombe. Watu walio karibu naye wameendelea kufichua kuwa Omosh ni mlevi chakari na amekataa kubadilika licha ya juhudi nyingi ambazo familia na marafiki wametia.

•Video moja ambayo inaonyesha mtu anayeaminika kuwa Omosh akiwa amelewa chakari ilienea sana mitandaoni asubuhi ya Jumatatu. Alionekana kulemewa kutembea na kusaidiwa na mwanaume mwingine aliyemshikilia asianguke.

Omosh
Omosh
Image: Hisani

Je, yepi yalimpata nyota wa Tahidi High?

Kipindi cha Tahidi High kilitumbuiza Wakenya sana miaka kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Kipindi hicho kilishirikisha baadhi ya waigizaji na watangazaji bora nchini wakiwemo Ken Wakuraya,Abel Mutua , Sarah Hassan miongoni mwa wengine.

Wengi wa waigizaji kwenye kipindi hicho waliendelea kubombea kwenye vitengo mbalimbali vya usanii baada ya kuondoka pale.

Hata hivyo, kunao baadhi yao ambao hawakuweza kustawi baada ya kuondoka Tahidi High. Mmoja wao ambaye ameibua gumzo mitandaoni ni Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh.

Madai yameibuka kuwa mwigizaji huyo alizama kwenye uraibu wa pombe. Watu walio karibu naye wameendelea kufichua kuwa Omosh ni mlevi chakari na amekataa kubadilika licha ya juhudi nyingi ambazo familia na marafiki wametia.

Video moja ambayo inaonyesha mtu anayeaminika kuwa Omosh akiwa amelewa chakari ilienea sana mitandaoni asubuhi ya Jumatatu. Alionekana kuchechemea na kuhitaji usaidizi wa  mtu mwingine kuweza kutembea.

Wanamitandao wameendelea kuashiria ghadhabu na Omosh kufuatia kufichuka kwa video hiyo huku wengi wakipendekeza apelekwe katika  kituo cha kurekebisha mienendo ili aweze kupambana na uraibu wa pombe.

Hizi hapa hisia za baadhi ya Wakenya mitandaoni:

Wasanii wenzake ikiwemo waliokuwa wanaigiza naye katika kipindi cha Tahidi High wameeleza kuwa Omosh ni mraibu wa pombe na juhudi za kurekebisha tabia zake hazijafua dafu kufikia sasa.

Mmoja wa waigizaji wenzake kwenye kipindi cha Tahidi High, Kevin Onyiso almaarufu kama Freddy alifichua kuwa Omosh ana shida ya ulevi na anahitaji kusaidiwa. Alipendekeza mwenzake apelekwe rehab kwani juhudi zake miezi kadhaa iliyopita ziliangulia patupu.

"Nilijaribu kumpigia simu vile alipata pesa, baada ya Shish kunipigia na kuniambia nimtafute kwani kuna watu wa NACADA walikuwa wamekubali kumpeleka rehab bila malipo. Hakuwa anachukua simu zangu na ikasemekana kuwa ana msaidizi. Nikapigia bibi yake nikamueleza kuwa waitumie fedha zile hadi wakati atakubali kuenda rehab ambako atarudi baada ya miezi mitatu akiwa sawa. 

La kuchekesha ni kuwa, jana nilimpigia simu na akaniambia kuwa bibi yake hakufikisha ujumbe  wa rehab na pia msaidizi wake hakumuarifu kuwa nimepiga.

Vile maji imezidi unga na hana hata shilingi tano ya sigara. Ni heri ashikwe na alazimishwe kuenda rehab kwani naona kitendo cha kujitia kitanzi kikija kwa umbali" Freddy alisema.