Omosh azungumzia video inayomuonyesha akiwa mlevi chakari na madai kuwa amefilisika

'Tunakula, tuko sawa, tunasonga mbele. Kitendo changu kupeana nambari nitumiwe pesa ilikuwa mzaha tu, lilikuwa jambo la kutumbuiza tu" Omosh alisema.

Muhtasari

•Akiwa kwenye mahojiano na Hiram Maina, Omosh aliwaomba Wakenya msamaha kufuatia video ambayo inaenea mitandaoni ambayo inamuonyesha akiomba pesa tena.

 

Omosh
Omosh
Image: Hisani

Aliyekuwa mwigizaji wa Tahidi High, Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh amekanusha madai kuwa amekuwa fukara tena.

Omosh pia amesema kuwa hajarejelea uraibu wa pombe na kuwa amekaa kwa muda bila kupiga maji.

Akiwa kwenye mahojiano na Hiram Maina, Omosh aliwaomba Wakenya msamaha kufuatia video ambayo inaenea mitandaoni ambayo inamuonyesha akiomba pesa tena.

Alisema kuwa maneno aliyosema kwenye video ya mahojiano ambayo inasambazwa mitandaoni yalikuwa ya kimzaha tu na hayakumaanisha kuwa amefilisika.

'Tunakula, tuko sawa, tunasonga mbele. Kitendo changu kupeana nambari nitumiwe pesa ilikuwa mzaha tu, lilikuwa jambo la kutumbuiza tu" Omosh alisema.

Hata hivyo, amesema kuwa ni kweli anahitaji camera ili aweze kutengeneza filamu zake.

"Naskia kuna watu kadhaa wananiambia kuwa wanaweza saidia. Wanaweza kuja tu wanisaidie na camera. Ni kweli nahitaji camera.. nahitaji kitu ambayo inatoa picha vizuri ndio kiwango cha uigizaji wangu kiwe juu" Omosh alisema

Hiram alimuahidi Omosh kuwa angewasiliana na msanii B Classic ambaye aliahidi kuwa atampatia camera.

Omosh pia alizungumzia uvumi unaoenea kuwa amerejelea uraibu wa pombe baada ya video ambayo ilionyesha akiwa mlevi  chakari kuenea mitandaoni.

Amesema kuwa video hiyo  ilirekodiwa wakati alikuwa ametoka kupiga sherehe aliyokuwa amealikwa na rafiki yake na si eti ni jambo analofanya kila siku. 

Alikiri kuwa msongo wa mawazo ulisababishwa na janga la Korona ulimfanya kurejelea ulevi licha ya kuwa amekoma kwa kipindi cha miaka miwili.

"Siwezi kudanganya ati niliwacha pombe. Kuna wakati nilikaa miaka 2-3 bila kunywa baada ya kutoka rehab. Lakini baada ya janga la Korona kuja nilijipata na msongo wa kimawazo na nikashawishiwa kunywa pombe mara kwa mara" Omosh alisema

Hata hivyo amesema kuwa hataki uhusiano wowote na pombe tena na akaagiza watu wasimnunulie pombe tena.

Omosh amesema kuwa ghadhabu ya Wakenya imemsaidia sana kurekebisha tabia zake 

"Wanaponikasirikia mimi sioni ghadhabu yao, naichukulia kama mawaidha" Alisema.

Aliwashukuru Wakenya kwa kumsaidia kujiinua tena na akawaagiza kumuombea asirejelee mienendo mibaya.