Miss Morgan ashauri Omosh kukubali kuwa anahitaji usaidizi kutatua shida ya uraibu wa pombe

,Amewasihi Wakenya kuelewa kuwa uraibu wa pombe ni ugonjwa na walioathirika wanahitaji usaidizi

Muhtasari

•Waruinge ambaye aliigiza kama naibu mwalimu mkuu kwenye kipindi hicho amemwambia Omosh kuwa hatua yake ya kujitokeza na kuomba  msaada wa fedha kwa mara nyingine kumesikitisha wengi.

•Alimsihi kubadilisha mienendo yake na awache kujihisi kama kwamba ako na haki ya kusidiwa na dunia.

Joseph Kinuthia, Angel Waruinge na Kamuhunjia
Joseph Kinuthia, Angel Waruinge na Kamuhunjia
Image: Instagram// Angel Waruinge

Angel Waruinge almaarufu kama Miss Morgan amemshauri aliyekuwa mwigizaji mwenzake kwenye kipindi cha Tahidi High, Joseph Kinuthia(Omosh) kukubali kuwa anahitajji usaidizi kutatua shida yake ya ulevi.

Waruinge ambaye aliigiza kama naibu mwalimu mkuu kwenye kipindi hicho amemwambia Omosh kuwa hatua yake ya kujitokeza na kuomba  msaada wa fedha kwa mara nyingine kumesikitisha wengi.

Kupitia akaunti yake ya YouTube, Waruinge ameeleza hasira yake kufuatia kile amesema ni kukosa shukrani kwake Omosh.

"Unasikitisha watu wengi. Wengi wetu tulikuwa katika hali hiyo pia. Wengine waliamua kukubali usaidizi na wakapata, wengine wakachagua kubadilika na wamebadilisha maisha yao, wengine waliamua kutojitosa kwenye uraibu wa pombe na wanastawi. Unaumiza watu wengi kutokana na yale unafanya" Waruinge alimwambia Omosh.

Alimwambia kuwa anaumiza jamii yake, Mungu, waliokuwa wenzake na pia anajiumiza yeye mwenyewe.

Waruinge ambaye pia alikuwa ameathirika na uraibu wa pombe amemtaka Omosh kukubali kusaidiwa kupambana na tatizo hilo 

"Nakusihi ukubali kuwa unahitaji msaada, lazima itoke kwako. Unaelewa kuwa asilimia 70% ya kupona inatoka kwako, asilimia nyingine unaweza pata kutoka kwa familia, marafiki na wengineo" Waruinge alimshauri Omosh.

Alimsihi kubadilisha mienendo yake na awache kujihisi kama kwamba ako na haki ya kusidiwa na dunia.

Mwigizaji huyo alikiri kuwa pia yeye amewahi kuwa mwathiriwa wa uraibu wa mihadarati na msongo wa mawazo na alipokea usaidizi kupambana na hali hiyo.

Hata hivyo, amewasihi Wakenya kuelewa kuwa uraibu wa pombe ni ugonjwa na walioathirika wanahitaji usaidizi.

"Kwa watu wote huku nje, tafadhali muelewa kuwa uraibu wa pombe ni ugonjwa.Tafadhali tuache matusi na kufuatilia familia na watu wengine ambao hawahusiki kwenye maisha yake" alisema Miss Morgan.