'Alilia tuende naye nyumbani' Bahati asimulia alivyompata mwanawe kutoka nyumba ya watoto

Morgan Bahati alikuwa na umri wa takriban miaka minne wakati Bahati alimchukua na kumfanya mwanawe

Muhtasari

•Morgan Bahati alikuwa na umri wa miaka miwili wakati Bahati alimchukua na kumfanya mwanawe. Alikuwa  amejiunga na ABC baada ya kupoteza  wazazi wake.

•Bahati pia alilimbikizia familia yake yote sifa wakiwemo mabinti wake wawili na bibi yake Diana Marua na kuitaja kama familia ya ajabu.

Image: INSTAGRAM

Mwanamuziki wa nyimbo za injili na mapenzi, Kevin Bahati amesimulia alivyopanga mtoto kutoka nyumba ya watoto ya ABC mtaa wa Mathare miaka kadhaa iliyopita.

Morgan Bahati alikuwa na umri wa takriban miaka minne wakati Bahati alimchukua na kumfanya mwanawe. Alikuwa  amejiunga na ABC baada ya kupoteza  wazazi wake.

Kulingana na mwanamuziki Bahati, Morgan alilia na kuomba waende naye kwake baada ya kutamatika kwa tamasha yake ya kwanza. 

Amesema kuwa Morgan hakutaka kurudi katika nyumba ya kutunza yatima ya ABC na akasisitiza kumfuata nyuma.

"Hii ilikuwa ngumu kwangu kwa kuwa nilijua ilivyomaanisha na ngumu zaidi kwa kuwa sikuwa katika hali nzuri kifedha singeweza kumudu kulea mtoto. Tatizo kubwa ni kuwa nilikuwa nikiishi kwa nyumba ndogo na sikuwa nimehitimu kupanga mtoto (Sikuwa na mtu wa kutunza mtoto huyo)" Bahati alisimulia.

Mwanamuziki huyo amesema kuwa ilibidi ajifunze kupika, kuandamana na mwanawe alipokuwa anaenda kufanya tamasha na kukosa kuchumbia wanawake kwa hofu ya kusababisha kuchanganyikiwa kwa mwanawe kuhusiana na atakayeita 'mama'.

"Tumepitia mengi nawe mwanangu ata nikikuona huwa siamini unaongea Kizungu safi kuniliko  aaii. Hili chapisho halitoshi kumwambia Mungu asante. Mungu amekuwa mwaminifu sana maishani mwetu, tuangalie sasa!!" Bahati aliandika.

Bahati pia alilimbikizia familia yake yote sifa wakiwemo mabinti wake wawili na bibi yake Diana Marua na kuitaja kama familia ya ajabu.

"Naweza kupa wakati na mapenzi yote unayohitaji kutoka kwa baba ila ukae ukikumbuka kuwa babako anakupenda" Bahati alimwandikia mwanawe.

Mwanamuziki Bahati alimpoteza mama yake mzazi akiwa na umri wa miaka 7. Hapo alijiunga na nyumba ya kuwatunza mayatima ya ABC ili kupata makazi na masomo.

Alimchukua Morgan akiwa na umri wa miaka 20 pekee.