Hatimaye nyumba yaaliyekuwa mwigizaji wa Tahidi High, Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh imekamilika.
Hafla ya kumkabidhi Omosh umiliki wa nyumba hiyo inatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano.
Wakitangaza kukamilika kwa nyumba hiyo kupitia mtandao wa Instagram siku ya Jumanne, wadhamini wa ujenzi wa nyumba hiyo Sung Timber & Products walishukuru Mungu na wote ambao walifanikisha kukamilika kwa ujenzi huo.
"Hatimaye tumekamilisha.. Omosh ndiyo hii zawadi yako maridadi... Niruhusu nimshukuru Mungu na timu ambayo ilifanikisha haya. Nimewavulia kofia. Shukrani maalum kwa mkandarasi wetu kwa kuzidia matarajio yetu" Sung Timber waliandika.
Mtangazaji na mcheshi Jalang'o ambaye alisaidia pakubwa katika kujumuisha wadhamini wa ujenzi wa nyumba alitangaza kuwa Omosh atakabidhiwa umiliki wa nyumba huyo Jumatano.
"Nyumba ya Omosh hatimaye imekamilika! Kesho tunakabidhiana nyumba!" Jalang'o alisema.
Wadhamini walijumuika na kujitolea kujengea Omosh nyumba baada yake kusimulia shida zilizokuwa zimempata.
Ujenzi wa nyumba hiyo ulifanikishwa na wadhamini kadhaa ikiwemo Sung Timber, Safina Furniture Enterprises, KPipes and Fittings na wengineo baada ya Omosh kusimulia masaibu yaliyokuwa yamemkumba.
Alikuwa ameomba Wakenya kumsaidia kujiinua tena huku akisema kuwa hakuwa na kazi na alikuwa amefirisika.