"Naamka saa tisa vilio na maumivu" Babu Tale aomba usaidizi kupambana na majonzi ya kufiwa na mkewe

Tale ambaye ni meneja wa msanii Diamond Platnumz amesema kuwa ingawa hajawahi kutamani kukutana na mwanasaikolojia ila kwa sasa yuko tayari kusaidiwa kupambana na hali ile.

Muhtasari

•Kupitia mtandao wa Instagram, Tale ambaye pia ni mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki amesema kuwa hayuko katika hali nzuri kwani anamkumbuka sana marehemu mke wake

Image: INSTAGRAM

Meneja wa staa wa Bongo Diamond Platnumz, Hamisi Taletale almaarufu kama Babu Tale amekiri kuwa anahitaji  usaidizi wa mwanasaikolojia kutokana na wakati mgumu ambao anapitia kwa sasa kufuatia kifo cha mke wake.

Kupitia mtandao wa Instagram, Tale ambaye pia ni mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki amesema kuwa hayuko katika hali nzuri kwani anamkumbuka sana marehemu mke wake.

Amesema kuwa ingawa hajawahi kutamani kukutana na mwanasaikolojia, kwa sasa yuko tayari  kusaidiwa kupambana na hali ile.

"Sijawahi kutamani kukutana na mwana saikojia ila kwa sasa nahitaji kwakweli maana hali yangu sio nzuri kwenye hiki ninachopitia namkumbuka sana mkewangu. Mungu aendelee kukulaza mahala pema Mama TT" Tale alisema.

Mkewe Tale aliyefahamika kama Shamsa Kombo (Shammy) aliaga dunia mnamo Juni mwaka uliopita na kuacha nyuma watoto watatu.

Babu Tale amefichua kuwa kwa kipindi cha siku tatu mtawalia sasa amekuwa akiamka saa tisa usiku kulia kutokana na maumivu makubwa.

"Kuna vitu omba visikukute katika maisha yako. Usiombe uondokewe na mke au mume. Mimi napitia maisha magumu sana kila ukiona unakaribia kukaa sawa kumbe unajiona bado maumivu hayaishi maana leo nina siku ya tatu naamka tisa usiku vilio na maumivu yasio isha." Alisema Tale.

Mwishoni mwa mwezi uliopita Tale aliandamana na Diamond kuhudhuria hafla ya kutunza wasanii ya BET Awards 2021. Hata hivyo, msanii huyo hakutwaa ushindi wa tuzo hilo ambalo lilinyakuliwa na Burna Boy kutoka Nigeria.