'Mama yangu alinitupa chooni' Mwanamuziki Shalkido asimulia alivyoachwa na mamake akiwa na miezi 2

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo alisema kuwa nyanya yake ndiye alimnusuru baada ya mamake mzazi kumuacha ndani ya choo kufuatia mzozo na baba yake.

•Msanii huyo alieleza kuwa nyanya yake alichukua majukumu ya kumlea baada ya mama yake kutoweka na amekuwa akimuita 'mama'

Image: INSTAGRAM// SHALKIDO GA CUCU

Mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo aina ya Gengetone na Mugithi Shalkido amefunguka kuhusu maisha yake ya utotoni na jinsi alitengwa na mama yake akiwa angali mdogo mno.

Akiwa kwenye mahojiano na Ala C katika kipindi cha 'Reke Ciume na Ene' kwenye mtandao wa YouTube, msanii huyo ambaye alitambulika sana akiwa kwenye kundi la Sailors alifichua kuwa amelelewa na nyanya yake baada ya kuachwa na mama yake akiwa na umri wa miezi miwili tu.

"Mimi nimezaliwa Matangini, Ruiru. Watu hujiuliza mbona huwa najiita 'Ga Cucu' (wa nyanya) ilhali sio nyanyangu aliyenizaa. Niko na hadithi refu ya maisha yangu na yenye machungu mengi. Mamangu aliniacha nikiwa na miezi miwili tu" Shalkido alisema.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa nyanya yake ndiye alimnusuru baada ya mamake mzazi kumuacha ndani ya choo kufuatia mzozo na baba yake.

Alidai kuwa anafikiri baba yake alikuwa na tamaa kubwa ya wanawake huenda jambo hilo lilichangia kutengana kwa wazazi wake.

"Nafikiri babangu alikuwa anapenda wanawake sana na nadhani ndio maana walikosana na mama yangu akaamua kuenda. Aliacha kama amenifunga na leso akanitupa kwa choo. Nyanyangu alipokuwa shambani akashangaa kwani mtoto amekuwa wa miujiza. Inakuwaje mtoto wa miezi miwili anaweza kujipeleka choo? Akaja akanichukua" Shalkido aliambia Ala C.

Msanii huyo alieleza kuwa nyanya yake alichukua majukumu ya kumlea baada ya mama yake kutoweka na amekuwa akimuita 'mama'

"Nyanya aliponichukua  kutoka pale kwa choo akachukua majukumu ya kunilea kwa hivyo nilikua kama namuita 'mama'. Mara nyingi  nilikuwa namuuiliza inakuwaje babangu anamuita mama nami pia namuita vile.. Hakuta kuzungumzia suala lile ila siku moja ilifika ikabidi aniambie" Shalkido alisimulia.

Alisema kuwa licha ya yote aliyopitia angependa sana kumuona mama yake na kumfahamu vizuri ajue sababu zake kumuacha.

"Naweza penda kujua mamangu. Popote ulipo nakutafuta. Ningependa kumuuliza nilimfanyia nini akaamua kuniacha na  machungu yale. Nilifanya nini na nilikuwa mtoto mdogo aliyekuwa amezaliwa juzi juzi tu" Shalkido alisema.

Hata hivyo mwanamuziki huyo hajuti maamuzi ya mamake mzazi kumuacha akiwa mdogo na ameapa kuwa iwapo angempata anaweza kumtuza vizuri.

"Najua mama yangu alipo ananitazama. Ulifanya vizuri, Mungu akubariki. Tutapana mahali nikununulie nyama na nikujengee. Mabaya ya mtu hulipwa na mazuri" Alisema Shalkido.

Msanii huyo alifichua kuwa amepitia maisha magumu kabla afike alipo kwa sasa.