Mfahamu Jean-Pierre Adams, mwanasoka aliyekuwa katika koma kwa miaka 39; Nini kilitokea akapoteza fahamu?

Mwaka wa 1982 Adams alipokuwa akishiriki mazoezi na klabu ya Chalon alipata jeraha lililomlazimu kulazwa katika hospitali ya Édouard Herriot

Muhtasari

•Kifo cha Adams kilithibitishwa asubuhi ya Jumatatu na hospitali ya chuo kikuu cha Nimes baada yake kukosa fahamu kwa kipindi cha miaka 39.

•Alichezea timu ya taifa ya Ufaransa kati ya mwaka wa 1972 na 1976 na kushiriki kwenye mechi 22.

Jean-Pierre Adams
Jean-Pierre Adams
Image: GETTY IMAGES

Siku ya Jumatatu (Septemba 7, 2021) habari kuhusu kifo cha mwanasoka wa zamani wa timu ya kitaifa ya Ufaransa Jean-Pierre Adams (73) ambaye alikuwa katika koma tangu 1982 ziligonga vichwa vya habari.

Kifo cha Adams kilithibitishwa asubuhi ya Jumatatu na hospitali ya chuo kikuu cha Nimes baada yake kukosa fahamu kwa kipindi cha miaka 39.

Adams alishiriki kwenye mechi yake ya mwisho takriban miongo minne iliyopita na hayo huenda wengi hawamfahamu.

Kuzaliwa

Je, Pierre Adams ni nani? Alizaliwa lini? Alichezea klabu zipi? Je nini kilitokea akajipata katika hali ile kwa miaka 39?

Marehemu Jean-Pierre Adams alizaliwa mwaka wa mano Machi 10, 1948 jijini Dakar, Senegal. Alilelewa pale Senegal hadi alipofikisha miaka 10 ambapo aliandamana na nyanya yake kuelekea Ufaransa.

Adams alipofika Ufaransa alichukuliwa na wanandoa Wafaransa ambao walimtunza kama mtoto wao na kumpeleka shule.

Kucheza kwake 

Talanta ya Adams ya kucheza soka iligunduliwa alipokuwa anasoma  na akaanza kuchezea klabu ndogo ndogo maeneo ya Lorient, Ufaransa.

Aliaanza taaluma ya kucheza soka  mwaka wa 1967 katika klabu ya Entente Bagneaux-Fontainebleau-Nemours nchini Ufaransa.

Miaka mitatu baadae beki huyo alisajiliwa na klabu ya Nimes ambayo alichezea hadi mwaka wa 1973 alipojiunga na Nice. Alipokuwa Nimes, Adams alishirikishwa kwenye mechi 84.

Adams alichezea Nice kwa miaka minne alikoshiriki katika mechi zaidi ya 120 na kufunga mabao 15 kabla ya kujiunga na PSG mwaka wa 1977.

Mchezaji huyo alichezea miamba hao wa soka Ufaransa kwa miaka miwili na kushirikishwa kwenye mechi 40.

Adams pia alichezea klabu za Mulhouse na Chalon kabla ya kufanyiwa upasuaji uliomuacha bila fahamu mwaka wa 1982.

Alichezea timu ya taifa ya Ufaransa kati ya mwaka wa 1972 na 1976 na kushiriki kwenye mechi 22.

 Nini kilitokea Adams akapoteza fahamu kwa miaka 39

Mwaka wa 1982 Adams alipokuwa akishiriki mazoezi na klabu ya Chalon  alipata jeraha lililomlazimu kulazwa katika hospitali ya  Édouard Herriot.

Adams alipokuwa amelazwa hospitalini alifanyiwa upasuaji kwenye goti lake mnamo Machi 17, 198   lakini hakupata tena ufahamu baada ya makosa ya daktari aliyemdunga sindano ya kulała.

Upasuaji wake ulifanyika huku daktari aliyehusika na kudunga sindano ya ganzi akihudumia wagonjwa wanane , ikiwemo Adams wakati huo mmoja.

Siku ambayo Adams alifanyiwa upasuaji huo wafanyakazi wengi wa hospitali katika klabu ya Chalon walikuwa katika mgomo.

Kabla ya upasuaji uliomletea madhara yale kufanyiwa, Adams aliripotiwa kuwa mzima na tayari kufanyiwa upasuaji.

Tangu  apoteze fahamu  miaka 39 iliyopita, Adams amekuwa akihudumiwa na mkewe Bernadette ambaye walifunga ndoa naye mwaka wa 1969 na kubarikiwa na watoto wawili.

Kuaga dunia.

Kifo cha Adams kilitangazwa mnamo Septemba 6, 2021, habari ambazo zilithibitishwa na magazeti nchini Ufaransa.

Alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 73.