Ni ujinga tu! Mchekeshaji Jalang'o akana kupokea pesa kutoka kwa jamaa aliyeapa kurejesha msaada wake

Mwezi uliopita Jalang'o alisaidia Felix Mboya 21, kumaliza kulipa deni ya kodi ya nyumba ya shilingi 18,000 ambayo alikuwa ameshindwa kulipa.

Muhtasari

•Mboya alionekana kutoridhishwa na ushauri wa Jalang'o na wiki kadhaa baadae akatishia kurejesha msaada ambao alikuwa amepokea.

•Jalang'o amejitokeza kukanusha madai hayo akidai kuwa jamaa yule anatafuta kiki tu kwani anapanga kutoa ngoma.

Image: INSTAGRAM

Mchekeshaji maarufu nchini Felix Odiwour almaarufu Jalang'o amefichua kuwa hajapokea pesa zozote kutoka kwa jamaa ambaye alisaidia kulipa kodi ya nyumba.

Mwezi uliopita Jalang'o alimsaidia Felix Mboya 21, kumaliza kulipa deni ya kodi ya nyumba ya shilingi 18,000 ambayo alikuwa ameshindwa kulipa.

Jalang'o pia alimshauri jamaa huyo achape kazi ili ajitegemee na aache kutafuta huruma kutoka kwa watu wengine.

Hata hivyo, Mboya alionekana kutoridhishwa na ushauri wa Jalang'o na wiki kadhaa baadae akatishia kurejesha msaada ambao alikuwa amepokea kutoka kwa Jalang'o.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Mboya alipakia picha iliyoonyesha ujumbe wa 'Mpesa' ukidai kumtumia Jalang'o shilingi 18000.

"Shukran sana kwa msaada wako natumai kuwa umeweza kupokea pesa zako sasa Heavy J" Mboya aliandika.

Hata hivyo Jalang'o amejitokeza kukanusha madai hayo akidai kuwa jamaa yule anatafuta kiki tu kwani anapanga kutoa ngoma.

Kulingana na Jalang'o, ujumbe wa Mpesa ambao kijana yule alipakia ulikuwa ghushi na hakuna pesa zozote ambazo amepokea.

"Kama kiki ni mtu! Waaah! Nimezungumza na kijana huyu aache kutumia jina langu kutafuta kiki! Huu ni ujumbe ambao umeghushiwa! Naweza kudhibitisha kuwa hakuna pesa ambazo amenitumia. Ni ujinga tu! " Jalang'o amesema.

Mfanyibiashara huyo  alisema kuwa anasikitika kuona kuwa kijana aliyekuja kwake akimlilia ili  amsaidia kulipa deni amebadilika ghafla na 'hayawani'

"Natumai kuwa siku moja atafahamu kwamba kuna watu wanatamani iwapo wangeweza kupata pesa ambazo nilimpatia kwa uaminifu. Siwezi amini kuwa huyu ni yule kijana ambaye alikuja kwangu akilia na sasa amebadilika kuwa hayawani. Nimemuonya dhidi ya kutumia jina langu kutafuta kiki.. anasema ni ngoma anataka kutoa" Amesema Jalang'o.

Wanamitandao wengi wamejitokeza kukashifu matendo ya Mboya huku wengi wakimshauri ajifunze kuwa mwenye shukrani.