"Niliugua TB kwa kutumia sigara na pombe" Kabi afunguka kuhusu maisha yake katika uasherati, uraibu wa mihadarati kabla ya kuokoka

Siku ambayo alienda kanisani kuokoka alikuwa amelala kwa baa akibugia mvinyo

Muhtasari

•Kupitia mtandao wa YouTube, Kabi alifichua kwamba kabla akubali kumkabidhi Yesu maisha yake alijihusisha na mienendo isiyo ya kimaadili kama vile uasherati na utumizi wa madawa ya kulevya.

•Kabi alifichua kwamba wakati alijiunga na chuo kikuu tayari alikuwa mraibu wa bangi na angeraukia msokoto kila asubuhi kama kiamsha kinywa. 

•Alikiri kwamba kwa wakati mmoja alikuwa amejitosa kwenye uraibu wa pombe, sigara, bangi na mihadarati mingine hadi akapatwa na matatizo ya kiafya

Image: INSTAGRAM// KABI WAJESUS

Siku ya Jumatano, Septemba 15 mwanavlogu na mchekeshaji mashuhuri nchini Peter Kabi almaarufu kama Kabi Wajesus aliadhimisha miaka 8 ya wokovu.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 30 alimkabidhi Yesu maisha yake mnamo Septemba 15 mwaka wa 2013 katika kanisa ya CITAM.

Kabi alitumia fursa ya kusherehekea miaka 8 tangu alipookoka kufunguka kuhusu maisha yake ya hapo awali.

Kupitia mtandao wa YouTube, Kabi alifichua kwamba kabla akubali kumkabidhi Yesu maisha yake alijihusisha na mienendo isiyo ya kimaadili kama vile uasherati na utumizi wa madawa ya kulevya.

"Niko na hadithi nyingi kama vile nilijitosa kwa uasherati, unywaji wa pombe, nikaingia sana kwa wasichana... nilikuwa na wasichana wengi, wapenzi wengi, nilikuwa nafanya hizo vituko vyote kama 'threesomes' kwani sikuwa na mtu wa kunishauri vizuri" Kabi alisema.

Mwanavlogu huyo alifichua kwamba alitumia bangi kwa mara ya kwanza akiwa katika darasa la tano baada ya kushawishiwa na rafiki yake.

"Tulivuta bangi kisha nikaambia binamu yangu ambaye alienda akafahamisha mama yangu. Mamangu alilia huku akiniambia sifai kuvuta bangi. Aliniambia alikuwa na matumaini mengi kwangu na alitaka sana nifaulu. Hapo nikaamua kuacha kuvuta bangi ili kuheshimu mama yangu" Kabi alisimulia.

Image: INSTAGRAM// KABI WAJESUS

Baada ya kuacha kutumia bangi kwa muda, Kabi alijitosa kwenye unywaji wa pombe kisha akarejelea utumizi wa bangi akiwa katika kidato cha kwanza.

Kabi alifichua kwamba wakati alijiunga na chuo kikuu tayari alikuwa mraibu wa bangi na angeraukia msokoto kila asubuhi kama kiamsha kinywa. 

"Kitu cha kwanza nilikuwa nafanya hata kabla nifungue macho ni kutafuta bangi yangu na kuiwasha ili nisikumbuke yale nilifanya usiku uliopita ama mtu ambaye nilikuwa nimegeuka kuwa" Kabi alisema.

Alisimulia kisa kimoja ambapo alivuta kiasi kikubwa cha bangi hadi akapoteza fahamu akiwa na nia ya kufahamu kile ambacho kingemtendekea.

"Nilikuwa nimeamua  kama ile bangi ingenipeleka vibaya ningewacha lakini  nisipofariki nitaendelea" Alisema.

Alipopoteza fahamu alianza kulia na kuomba Mungu amnusuru kutoka kwa hali huku akimuahidi kwamba angeacha kutumia bangi.

"Nilihisi kama nimeshikwa mateka. Niliomba Mungu aniwezeshe kulala na nikamuahidi ningemtumikia. Hatimaye nililala mida ya saa kumi asubuhi na nikaamka kitu saa tano. Hiyo siku nikaamua sitaki tena kuvuta bangi ila sikuokoka.. Baada ya miezi sita nikarejelea tabia ile" Kabi alisimulia.

Kabi alifichua kwamba wakati alijiunga na chuo kikuu tayari alikuwa mraibu wa bangi na angeraukia msokoto kila asubuhi kama kiamsha kinywa.

 "Niliacha pombe kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa sababu niliugua kifua kikuu. Niliugua TB nikiwa mdogo kwa sababu ya kuvuta sigara na kutumia pombe. Kinga ya mwili ilikuwa chini. TB ilinifanya niache pombe kwa kipindi cha mwaka mmoja lakini baada ya kupona nikarejelea pombe na bangi. Bangi ata sikuwa nimeacha, nilikuwa navuta bangi na  nakunywa dawa za TB" Kabi alisimulia.

Kabi alisema kwamba aliamua kuokoka miezi kadhaa baadae katika kanisa moja iliyokuwa karibu na mahali alikuwa anaishi.

Siku ambayo alienda kanisani kuokoka alikuwa amelala kwa baa akibugia mvinyo.

Alisema kwamba wengi hawakuamini alipotangaza kuwa ameokoka.