The Wa Jesus wasimulia walivyojuana kupitia rafiki wa Kabi aliyekuwa anachumbia Milly

Muhtasari

•Wawili hao walipatana kwenye hafla ya kuzindua nyumba ambayo Kabi alikuwa amealikwa kupiga picha na aliyekuwa mpenzi wa Milly kwa wakati huo.

•Baada ya kujuana, wawili hao walianza kuwa na uhusiano wa ndugu na dada kwani Milly bado alikuwa mpenzi wa rafikiye Kabi.

•Baada ya Milly kukamilisha masomo yake ya sekondari walikosana na mpenzi wake na kufuatia hayo mawasiliano kati yake na Kabi pia yalikatika.

Kabi na Milly Wajesus
Kabi na Milly Wajesus
Image: Instagram

Wapenzi wawili Kabi na Milly wa Jesus wamefunguka kuhusu walipopatana kwa mara ya ya kwanza.

Wakiwa kwenye mahojiano na  Mungai Eve, wawili hao walisema kuwa walipatana kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012. Kwa wakati huo Kabi alikuwa mpiga picha naye Milly alikuwa mwanafunzi wa kidato cha pili.

Wawili hao walipatana kwenye hafla ya kuzindua nyumba ambayo Kabi alikuwa amealikwa kupiga picha na aliyekuwa mpenzi wa Milly kwa wakati huo.

"Mwaka wa 2012 nilikuwa katika kidato cha pili na nilikuwa nachumbia rafiki wa Kabi. Hivo ndivyo tulipatana. Tulikuwa na hafla ya kuzindua nyumba na mpenzi wangu kwa wakati huo akasema kwamba anajua rafikiye ambaye angekuja atupige picha. Rafiki huyo alikuwa Kabi" Milly alisema. 

Milly alisema kuwa hakuwahi chumbia mtu mwenye umri sawa na yeye kwani pia mpenzi wake kwa wakati huo alikuwa ashamaliza masomo ya Sekondari.

Baada ya kujuana, wawili hao walianza kuwa na uhusiano wa ndugu na dada kwani Milly bado alikuwa mpenzi wa rafikiye Kabi.

Kabi alifichua kwamba alikuwa anamsaidia rafiki yake kuandikia mpenzi wake (Milly) barua akiwa sshuleni hadi alimaliza kidato cha nne.

Baada ya Milly kukamilisha masomo yake ya sekondari walikosana na mpenzi wake na kufuatia hayo mawasiliano kati yake na Kabi pia yalikatika.

"Baada ya kumaliza shule mawasiliano kati yetu yalikatika na pia tulikuwa tumekosana na mpenzi wangu kwa hivyo hatungeendelea kuwa marafiki na Kabi" Milly alisema.

Wawili hao waliwasiliana tena  baada ya miaka minne kupitia mtandao wa Facebook wakati Milly alikuwa anaendeleza masomo yake katika chuo kikuu.

"Nilipokuwa katika mwaka wa pili nikaona Kabi kwa mtandao wa Facebook. Nilimtambua kwani alikuwa amebadilisha jina na sura yake. Nikaingia kwa ukurasa wake nikaona ni kama alikuwa ameokoka. Nilipomuona kwa mara ya kwanza hakuwa mtu mzuri" Milly Alisema.

Hapo ndipo wakaanza kuwasiliana tena na kisha wakaanza kuchumbiana.