"Ni kama nitakufa" Ringtone adai kuwa aliathirika vibaya baada ya kupigwa rungu na Robert Alai

Muhtasari

•Ringtone amedai kwamba anapanga kuenda hospitalini kufanyiwa upasuaji kwani amekuwa akiumwa sana na kichwa hadi anakosa usingizi.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwanamuziki Alex Apoko amesihi mashabiki wake kumkumbuka kwa maombi akidai kuwa amekabiliwa na maumivu mabaya kichwani kufuatia vita kati yake na mwanablogu Robert Alai takriban miezi miwili iliyopita.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ringtone amedai kwamba aliathirika vibaya baada ya kugongwa kwa rungu kichwani na Alai mwezi Julai.

Ringtone amedai kwamba anapanga kuenda hospitalini kufanyiwa upasuaji kwani amekuwa akiumwa sana na kichwa hadi anakosa usingizi.

"Najaribu kufanya mazoezi. Kichwa kinauma,sijalala.Ile rungu niligongwa hapa iliniathiri. Nataka kuenda kufanyiwa upasuaji. Mniombee, sioni kama nitaponea, ni kama nitakufa. Niombeeni" Ringtone alisema.

Hata hivyo msanii huyo wa nyimbo za injili ameeleza matumaini yake kuwa Mungu atamponya  huku akidai kwamba iwapo atafariki, mwanablogu aliyempiga rungu ndiye atakuwa amesababisha kifo chake.

Miezi miwili iliyopika msanii huyo alidai kuwa alienda hadi Afrika Kusini kupokea matibabu maalum kufuatia mvurugano ambao ulifanyika katika barabara moja jijini Nairobi.

Mwanamuziki huyo ambaye anajitambulisha kama mwenyekiti wa  muungano wa wanamuziki wa nyimbo za injili alimshtaki Alai kwa kusababisha madhara mwilini wake na kuvunja kioo cha gari yake aina ya Range Rover wakati walikuwa wanazozana.