"Wanifanya nijihisi kama binti ya mfalme" Milly Wajesus asifia mapenzi makubwa anayopokea kutoka kwa mumewe Kabi

Muhtasari

•Milly Wa Jesus amemhakikishia mumewe Peter Kabi kuwa anampenda sana na ataendelea kumpatia mapenzi yake yote siku zote za maisha yake.

•Milly aliomba Mola awajalie fanaka kwenye ndoa yao mwaka huu na kuwawezesha kutengeneza kumbukumbu zaidi za mapenzi.

•Siku kadhaa zilizopita wawili hao walifichua jinsi walivyojuana kwa mara ya kwanza kupitia kwa rafiki wa Kabi ambaye alikuwa anachumbia Milly

Image: INSTAGRAM// MILLY WAJESUS

Mwanavlogu Millicent Wambui almaarufu kama Milly Wa Jesus amemhakikishia mumewe Peter Kabi kuwa anampenda sana na ataendelea kumpatia mapenzi yake yote siku zote za maisha yake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Milly amedai kwamba mumewe humfanya ajihisi kama binti ya mfalme kutokana na mapenzi makubwa anayomuonyesha.

Milly amesifia upendo wa Kabi na kupendezwa na jinsi huwa anamjali kama mpenzi wake.

"Nikiwa karibu nawe huwa najihisi kama binti ya mfalme. Wewe ni mwenye upendo na mwenye kujali kwa wakati mwingine. Sijui nilichokifanya ili nistahili kupata mapenzi kama haya lakini namshukuru Yesu. Nitaendelea kukupenda mfalme wangu @kabiwajesus" Milly alimwandikia mumewe.

Milly aliomba Mola awajalie fanaka kwenye ndoa yao mwaka huu na kuwawezesha kutengeneza kumbukumbu zaidi za mapenzi.

Siku kadhaa zilizopita wawili hao walifichua jinsi walivyojuana kwa mara ya kwanza kupitia kwa rafiki wa Kabi ambaye alikuwa anachumbia Milly.

Wapenzi hao ambao walifunga ndoa takriban miaka minne iliyopita walifichua kuwa walipatana kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012, Milly akiwa katika kidato cha pili.

Wanandoa hao walipatana kwenye hafla ya kuzindua nyumba ambayo Kabi alikuwa amealikwa kupiga picha na aliyekuwa mpenzi wa Milly kwa wakati huo.

Mwaka wa 2012 nilikuwa katika kidato cha pili na nilikuwa nachumbia rafiki wa Kabi. Hivo ndivyo tulipatana. Tulikuwa na hafla ya kuzindua nyumba na mpenzi wangu kwa wakati huo akasema kwamba anajua rafikiye ambaye angekuja atupige picha. Rafiki huyo alikuwa Kabi" Milly alisema.

Baada ya kujuana, wawili hao walianza kuwa na uhusiano wa ndugu na dada kwani Milly bado alikuwa mpenzi wa rafikiye Kabi.

Wakati Milly kukamilisha masomo yake ya sekondari walikosana na mpenzi wake na kufuatia hayo mawasiliano kati yake na Kabi pia yalikatika.

"Baada ya kumaliza shule mawasiliano kati yetu yalikatika na pia tulikuwa tumekosana na mpenzi wangu kwa hivyo hatungeendelea kuwa marafiki na Kabi" Milly alisema.

Wawili hao waliwasiliana tena  baada ya miaka minne kupitia mtandao wa Facebook wakati Milly alikuwa anaendeleza masomo yake katika chuo kikuu.

Wanavlogu hao walifunga pingu za maisha mwezi Desemba mwaka wa 2017.