"Nilitazama mume wangu akibisha mlango wa kifo" Nana Owiti asimulia masaibu yaliyompata wakati King Kaka alikuwa anaugua miezi 3

Muhtasari

•Baba huyo wa watoto watatu alisema kuwa kwa wakati huo alikuwa anakabiliana na kifo akitumai kupata nafasi nyingine ya kuwa na familia yake .

•Bi Owiti alifichua kuwa hali ya afya ya mpenzi wake iliendelea kumtia hofu zaidi siku baada ya nyingine haswa alipomtazama akiteseka kutokana na maumivu.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Siku ya Jumatatu mwanamuziki Kennedy Ombima maarufu kama King Kaka pamoja na mpenzi wake Nana Owiti walifunguka kuhusu nyakati ngumu ambazo walipitia wakati rapa huyo alikuwa amelemewa na maradhi ambayo yalimfanya apoteze zaidi ya kilo 33.

Staa huyo wa nyimbo za kufoka alipakia picha iliyoonyesha akiwa amedhoofika na kueleza kuwa ilipigwa punde  baada ya madaktari kumfanyia upasuaji kwenye mfupa wa nyonga , siku mbili tu  baada yake kulazwa hospitalini.

Baba huyo wa watoto watatu alisema kuwa kwa wakati huo alikuwa anakabiliana na kifo akitumai kupata nafasi nyingine ya kuwa na familia yake .

"Nilikuwa katikati ya dunia mbili nikipambana nione familia yangu tena. Ningelazimisha tabasamu wakati Nana na mama yangu walikuja kuniona lakini ukweli ni kuwa usiku ungepata giza zaidi na ningerudi kupigania maisha yangu" King Kaka alieleza.

Alisema kwamba ingawa bado hajapata afueni kabisa, anamshukuru Mola kwa kumjalia baraka ya uhai kuona kuwa anaweza kuamka na kula chakula chake mwenyewe.

Kwa upande wake Nana Owiti alisema kuwa wakati mumewe alikuwa anaugua ndio wakati mgumu zaidi amewahi kupitia maishani.

Alifichua kuwa hali ya afya ya mpenzi wake iliendelea kumtia hofu zaidi siku baada ya nyingine haswa alipomtazama akiteseka kutokana na maumivu.

"Kila siku nilidhani nimeona mabaya ila ninaona mabaya zaidi siku ifuatayo.. nilitazama mume wangu akibisha mlango wa kifo ila alivalia upendo wa Mungu. Labda aligonga mlango ili amfukuze shetani. Kusema kweli @thekingkaka alipigana vita" Bi Owiti alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Owiti alisema kuwa mumewe hakufa moyo licha ya kuzorota kwa afya yake na aliendelea kupigania maisha yake kwa ujasiri hadi alipoanza kuona mwangaza tena.

King Kaka alimshukuru sana mkewe, mama yake, ndugu zake, marafiki na mashabiki kwa kusimama naye katika wakati huo mgumu. Pia aliwashukuru madaktari ambao walimhudumia hospitalini hadi akapatiwa ruhusa ya kurudi nyumbani.

Wanamitandao ikiwemo watu mashuhuri na wasanii wenzake wameendelea kumtumia rapa huyo jumbe za kumtakia afueni ya haraka.