Hatimaye mchekeshaji Eric Omondi ametangaza mshindi wa shoo yake ya mwisho ya Wife Material huku akidai kwamba harakati zake za kutafuta mke zimefika kikomo.
Omondi ametangaza kwamba mwanamitindo Monica Ayen kutoka Sudan Kusini ndiye aliyenasa moyo wake kwani alitimiza yote aliyokuwa anatafuta kwa mke.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, baba huyo wa mtoto mmoja anayejulikana ameapa kufunga ndoa na Bi Monica na kuishi maisha yake yote pamoja na yeye kwenye dhiki na faraja
"Monica Ayen-Omondi. Hongera kwa kushinda moyo wangu. Hongera kwa kushinda shoo ya mwisho ya Wife Material. Naahidi kukupatia mapenzi yangu yote. Nitakuheshimu. Nitakuheshimu kwa utu wangu wote. Naahidi kukulinda. Siwezi kusubiri kuanzisha familia pamoja nawe. Siwezi subiri kupata watoto warembo na wewe. Wewe sio tu mwanamitindo bali una moyo mzuri. Unanikamilisha kipenzi. Unanikamilisha mpenzi wangu" Eric alitangaza.
Mchekeshaji huyo alishukuru taifa la South Sudan kwa kumpa malkia wa ufalme wake huku akiahidi kumlinda na kumpatia mapenzi yasiyoisha.
Hali kadhalika Omondi amewashukuru wanadada wote ambao walishiriki kwenye mashindano hayo pamoja na walioipa shoo hiyo mafanikio
"@ayen_monica nakuahidi nitakuoa na niiishi maisha yetu yote pamoja na wewe. Nitasimama na wewe kwenye dhiki na faraja, Nakupenda" Omondi alimalizia kwa kuapa.
Onyesho la kwanza la shoo ya Wife Material lilifanyika mwezi Desemba mwaka uliopita na kulikuwa na onyesho la pili mnamo mwezi Machi mwakani kabla ya onyesho la mwisho kung'oa nanga wiki iliyopita.