'Umaarufu, pombe ziliniharibia mwelekeo wa maisha,' O.J afunguka kuhusu maisha yake Tahidi High na uraibu wake wa pombe

Muhtasari

•Mwigizaji huyo alifichua alipopata umaarufu mkubwa alianza kuponda raha na akazama kwenye uraibu wa pombe, jambo ambalo lilifanya akapoteze mwelekeo wa maisha.

•O.J alisema uraibu wake wa pombe ulichangiwa zaidi na maisha yake ya utotoni, umaarufu na hali ya kuwa mzazi.

•Alifichua kwamba waigizaji wenzake wa Tahidi High, Abel Mutua na Phil Karanja ambao wenyewe hawakuwa walevi walijaribu kumshauri aache pombe ile hakusikia  la mwadhini wala la mteka maji msikitini

Image: INSTAGRAM// DENNIS MUGO OJ

Mwigizaji Dennis Mugo almaarufu kama O.J amefunguka kuhusu maisha yake alipokuwa anaigiza katika kipindi cha Tahidi High miaka kadhaa iliyopita.

Alipokuwa kwenye mahojiano na 'Glow up with Makena', O.J alianza kuigiza katika kipindi cha Tahidi High alipokuwa anaendeleza masomo ya uandishi wa habari katika chuo kikuu cha Kenya Institute of Mass Communication. 

Alisema shoo hiyo ilikuwa changa wakati alianza kuigiza na waigizaji walikuwa wanapokea shilingi elfu tatu baada ya kila kipindi walichohusika.

"Tulikuwa tunalipwa elfu tatu kila kipindi. Wakati huo sikuwa nimepata jina bado nilikuwa kijana mdogo. Mwelekezaji alikuwa anakuandikia kipindi kimoja alafu unapata elfu tatu. Sikuwa najali kwa sababu nilikuwa bado nategemea pesa za mzazi na sikuwa na watoto na majukumu mengi kwani niliishi kwa mama yangu. Lakini kufikia wakati tulikuwa tunatoka tulikuwa tunalipwa kama 25k na saa hiyo ushatengeneza jina kwa hivyo unaigiza katika kila kipindi" O.J alisema.

O.J ambaye kwa sasa anafanya kazi katika serikali ya kaunti ya Embu aliendelea kung'aa katika taaluma ya uigizaji hadi akapokea tuzo la Chaguo la Teeniez mnamo mwaka wa 2010.

Mwigizaji huyo alifichua alipopata umaarufu mkubwa alianza kuponda raha na akazama kwenye uraibu wa pombe, jambo ambalo lilifanya akapoteze mwelekeo wa maisha.

"Nilikuwa naingia kwa baa nasema watu ata wasio na pesa zozote kwa mfuko wapatiwe pombe. Nilikuwa na pesa , niliona eti sina matumizi. Umaarufu ulifanya nione kama mimi ndio mdosi. Dhana hiyo iliharibu mwelekeo wangu wa maisha" O.J alisema.

O.J alieleza aliendelea kubugia vileo hata baada ya kuondoka Tahidi High na kupata kazi nyingine katika kampuni ya kutangaza.

Alifichua kuna wakati alikuwa amegeuka kuwa mraibu mkubwa kiasi cha kwamba alihitaji pombe ili aweze kufanya kazi.

"Kila nilipoingia kwa ofisi nilikuwa nahitaji pombe ili niweze kufikiria. Mdosi akiniambia eti wanahitaji wazo la ubunifu kuhusu bidhaa fulani nilikuwa naagiza pombe kwanza. Wakati huo Tahidi High ilikuwa imeisha nilikuwa nafanya kazi katika kampuni ya matangazo" O.J alisema.

O.J alisema uraibu wake wa pombe ulichangiwa zaidi na maisha yake ya utotoni, umaarufu na hali ya kuwa mzazi.

"Ilichangiwa sana na maisha yangu ya utotoni. Wakati niligeuka kuwa baba ikawa mbaya zaidi kwa sababu sikujua jinsi ya kuwa  baba. Kila kitu kingine nilichokuwa nafanya nilikuwa nimesomea. Sikuwa nimesomea umaarufu, hali hiyo iliniharibia maisha. Umaarufu na hali ya kuwa baba ziliniharibia maisha" O.J alisema.

Alifichua kwamba waigizaji wenzake wa Tahidi High, Abel Mutua na Phil Karanja ambao wenyewe hawakuwa walevi walijaribu kumshauri aache pombe ile hakusikia  la mwadhini wala la mteka maji msikitini.

Baba huyo wa mtoto mmoja alisema ingawa sasa ameweza kujiinua tena, angali anajuta sana kupoteza miaka mingi katika uraibu wa pombe.