"Diamond aliniambia siwezi mshinda kihela, kiserikali na uchawi!" Harmonize azungumzia masaibu yaliyomkumba akiwa Wasafi

Muhtasari

•Moja ya sababu ambazo Harmonize alitoa ni kuwa alipokuwa Wasafi Diamond angechukua asilimia 60 ya mapato yalitokana na muziki wake ilhali yeye angesalia na asilimia 40% tu ambazo angetumia kutengeneza muziki wake.

•Harmonize alifichua aliamua kujiita jeshi kutokana na masaibu ambayo yalimkumba alipokuwa Wasafi ikiwemo kubandikwa jina msaliti baada ya kuondoka.

Harmonize na Diamond
Harmonize na Diamond
Image: INSTAGRAM

Punde baada ya kurejea Tanzania kutoka ziara yake Marekani, Harmonize alifunguka kuhusu ugomvi wake na aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz.

Alipokuwa anahutubia wanahabari waliomlaki katika uwanja wa ndege, kwa mara ya kwanza Konde Boy alifichua sababu zake kuondoka Wasafi licha ya kuwa hiyo ndio lebo iliyomfungulia milango mikubwa katika taaluma  yake ya muziki.

Moja ya sababu ambazo Harmonize alitoa ni kuwa alipokuwa Wasafi Diamond angechukua asilimia 60 ya mapato yalitokana na muziki wake ilhali yeye angesalia na asilimia 40% tu ambazo angetumia kutengeneza muziki wake.

"Nilisaini mkataba wa miaka 10 WCB. Katika mkataba huyo, kila pesa ambazo nilikuwa napata, kwa mfano nikipata laki moja yeye alikuwa anachukua elfu sitini mimi nachukua arubaini. Nikifanya shoo nilipwe milioni 10 yeye alikuwa anachukua milioni sita mimi nachukua milioni nne. Katika milioni nne hiyo hiyo nilikuwa naidunduliza najiongeza kukuza muziki wangu" Harmonize alisema.

Alieleza kwamba jambo hilo halikumvunja  moyo kwani aliamini siku ingefika wakati  ambapo lebo ya WCB ingekuwa kubwa na imruhusu atoke akajitegemee mwenyewe.

Kando na hayo, Konde Boy alisema Diamond pamoja na mameneja wake walianza kumuonea gere wakati nyota yake ilianza kung'aa zaidi hadi akatangaza vita dhidi yake.

"Aliniambia eti 'mimi nikimpa mtu heshima yangu, asiponirudishia naichukua kinguvu. Unataka kushindana na mimi na huniwezi kiserikali, huniwezi kihela na huniwezi kiuchawi. Nipe mkono tushindane.' Mimi nilibaki nimeduwa nikajiuliza kama tumefikia hatua hiyo keshoye mtu angeweza kuniwekea sumu nikafa" Alisema Harmonize.

Harmonize alisema Diamond ana mazoea ya kukosana na wanamuziki wenzake pindi anapoona kama kwamba  wameanza kung'aa.

"Ukiangalia wasanii ambao wamegombana na Diamond. Walianza kugombana wakati walianza kung'aa. Wakiwa chini wanakuwa marafiki. Kwa mfano Cheta, alipokuwa pale chini alikuwa rafiki wake. Lakini alipoanza kung'aa akaanza kuambiwa eti atapitwa. Ommy Dimpoz vilevile na wasanii wengine. Msanii ambaye amewahi kung'aa Tanzania lazima awe amegombana na Diamond" Harmonize alisema.

Mmiliki huyo wa lebo ya Konde Music Worldwide alisema kwamba ni kawaida ya Diamond kujaribu kuwazuia wanamuziki wengine kung'aa zaidi yake.

Harmonize alifichua aliamua kujiita jeshi kutokana na masaibu ambayo yalimkumba alipokuwa Wasafi ikiwemo kubandikwa jina msaliti baada ya kuondoka.