MAONI

Tahadhari kabla ya hatari! Sababu za kwanini Zuchu anafaa kuepuka mahusiano na Diamond Platnumz

Suala kuu ni kuhusu historia mbaya ya Diamond na wanawake

Muhtasari

•Tayari Diamond ana watoto wanne na wanawake watatu tofauti ambao ni mwanamuziki Hamisa Mobetto kutoka Tanzania, mwanasoshalaiti Zari Hassan kutoka Uganda na mwanamuziki Tanasha Donna kutoka Kenya.

•Mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' pia anafaa afahamu kwamba mwanamuziki wa tajriba kama ya Diamond ana uwezo wa kuvutia wanadada chungu mzima.

Diamond Platnumz na Zuchu
Diamond Platnumz na Zuchu
Image: INSTAGRAM

Katika kipindi cha wiki kadhaa ambacho kimepita mojawapo wa suala ambalo limeangaziwa zaidi ni tetesi kuwa mwanamuziki Zuchu anachumbiana kisiri na bosi wake wa WCB Diamond Platnumz.

Ingawa mamake Zuchu, Khadija Kopa amejitokeza kupuuzilia mbali madai hayo, idadi kubwa ya wanamitandao bado wanaamini mastaa hao huenda wameamua kufanya jaribio la ndoa.

Hivi majuzi kigogo wa taarab Khadija Omar Kopa na ambaye ni mamake Zuchu alieleza kwamba uhusiano wa Diamond na Zuchu ni wa dada na ndugu huku akidai bosi wa WCB huwa anamchukulia  yeye kama mama yake.

 Bi Kopa alisema tayari amehoji bintiye kuhusu madai hayo na alimhakikishia kuwa Diamond amekuwa akionyesha heshima kubwa kwake na hakuna chochote kinachoendelea kati yao.

"Wakati ule Zuhura aliniambia Diamond anamheshimu sana na hajawahi hata siku  moja kuniambia vitu vya kipuzi. Nilishtuka maanake watu walikuwa wanavumisha kupita kiasi. Nilishangaa mbona walivumisha kupita kiasi. Mimi mwenyewe sikushughulika sana. Nilimuuliza Zuhura mbona watu walivumisha sana ama kuna kitu chochote. Aliniambia hamna wala hajawahi kuvunjiwa heshima hata siku moja. Mimi nilichukulia kama kitu cha kawaida" Alisema Khadija Kopa.

Hata hivyo, hatuwezi puuzilia kabisa madai hayo kwani mara nyingi mastaa hao wawili wameonekana kuwa na uhusiano usio wa kawaida kwa ndugu na dada.

Iwapo madai hayo ni ya kweli ni vyema Zuhura kufahamu vizuri hali ambayo anakusudia kujiweka na kutahadhari kabla ya hatari.

Suala kuu ni kuhusu historia isiyo ya kusifiwa  ya Diamond na wanawake. Nyota huyo wa muziki anaaminika kuchumbia wanadada zaidi ya kumi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika.

Tayari ana watoto wanne na wanawake watatu tofauti ambao ni mwanamuziki Hamisa Mobetto kutoka Tanzania, mwanasoshalaiti Zari Hassan kutoka Uganda na mwanamuziki Tanasha Donna kutoka Kenya.

Licha ya mahusiano yake na malkia hao kufikia hatua ya kupata familia, Diamond bado aliwatema kutokana na sababu ambazo hatuwezi kufahamu labda atuambie mwenyewe.

Zuchu anapaswa kuelewa kwamba yeye sio tofauti na wale wengine ambao Diamond amechumbia.  Licha ya urembo, umaarufu na ushawishi wao vidosho hao bado walitemwa.

Hakuna mahusiano ya Diamond ya hapo awali  ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka mitano. Hamissa Mobetto na Zari Hassan ndio walichumbiana na Simba kwa kipindi kirefu zaidi.

Mwimbaji huyo wa kibao 'Sukari' pia anafaa afahamu kwamba mwanamuziki wa tajriba kama ya Diamond ana uwezo wa kuvutia wanadada chungu mzima.

Mara nyingi wasanii wale kama wale wanapoenda kutumbuiza huwa wanajipata kwenye majaribu makubwa ya kutoka nje ya ndoa kwani wanadada wengi huwatongoza wakilenga mahusiano ya kimapenzi  na supastaa wao. 

Hakuna uhakikisho wowote kwamba Diamond akijitosa kwenye mahusiano na Zuchu ataweza kukwepa majaribio kama yale.

Hata hivyo Khadija Kopa hata hivyo alisema yuko radhi iwapo bintiye atafanya maamuzi ya kuolewa nyumba ndogo kwani dini yao ya Kiislamu inawaruhusu.

Kutokana na hayo huenda Zuchu akawa sawa na Diamond kwani hata ifikapo wakati alete mwanamke mwingine kwa boma huenda haitamsumbua sana.