Msanii nambari moja wa muziki wa kizazi kipya nchini Kenya, Otile Brown hatimaye alirejea nchini asubuhi ya Ijumaa baada ya kuwa na msururu wa matamasha mengi nchini Marekani.
Msanii huyo alipotua katika anga tua ya JKIA, tukio lisilo la kawaida lilitokea ambalo lilimfanya kutokwa na machozi kwa kulemewa na hisia.
Baada ya kukaribishwa na makumi ya wanahabari waliofurika na vipaza sauti na kamera, jamaa mmoja anayedhaniwa kuwa shabiki wake kindakindaki alimkaribia na kufungua bango hilo kubwa ambalo alikuwa amechora picha ya marehemu nyanyake Otile na kumpa.
Pindi msanii huyo alipoona picha ile na kutambua sura ya nyanyake, alishindwa kuzuia hisia zake ambapo alizamisha uso wake ndani ya viganja vya mikono yake kwa dakika kadhaa kabla ya kufuta machozi na kumwendea yule jamaa na kumpa kumbato.
Kwa mara kadhaa, otile amekuwa akisikika kwa wingi akimsifia marehemu nyanyake akisema kwamba bibi huyo ndiye aliyemlea na kumkuza enzi hizo maisha yakiwa magumu kwao.
Itakumbukwa mwezi mmoja uliopita alipotua Marekani, Otile alinunua mkufu wa madini ya almasi ambao ulikuwa na picha ya nyanya yake katikati na kupakia picha hiyo akisema kwamba amefarijika kumuenzi nyanyake hata kama hayuko hai.
Katika ziara hiyo, Brown alisifia majimbo mengi ya huko Marekani ambapo alisema majimbo mawili tu ndio pekee hakuuza tikiti zote.
Alimiminia sifa majimbo kama ya Minnesota, Dallas, Las Vegas miongoni mwa mengine ambayo mihemko ilikuwa mingi sana kutoka kwa mashabiki.