Kwa muda wa wiki kadhaa, mama Dangote hajakuwa akionekana sana hadharani, haswa katika kuchapisha vitu kwenye ukurasa wake wa Instagram kama ilivyo kawaida yake hapo awali.
Ukimya huu wake kwa kiasi Fulani uliwachanganya na kuwashushua watu, mpaka kufikia kiwango ambapo baadhi ya wanablogu walianza kuchapisha habari zile ambazo Mama Dangote ameziita za kupotosha kwamba yuko mahututi hospitalini.
Mwanablogu Mange Kimambi kwa muda wa wiki kadhaa amekuwa mstari wa mbele kuchapisha taarifa hizo kwamba Mama Dangote anaumwa, ana hali mbaya na yuko hoi hospitalini ndio maana haonekani mitandaoni.
Akipuuzilia mbali uvumi huo wa kupotosha, Mama Dangote amerejea mitandaoni kwa kupakia video ndogo ambayo ilimuonesha akiwa kwenye tafrija Fulani pamoja na familia yake wakiwa wanalisasambua kwelikweli kwenye jukwaa kwa minenguo ya aina yake.
Baadhi ya wadadisi walisema kuwa Mama Diamond alihudhuria katika shughuli ya mamake Romy Joms ambaye ni kaka wa kupanga wa Diamond na DJ wake rasmi.
Walikuwa familia nzima kwa maana ya Romy Jons mwenyewe, Mama Dangote, mpenzi wake Uncle Shamte, Diamond miongoni mwa wanafamilia wengine.
Kwenye klipu hiyo, Mama Dangote alionekana mwingi wa afya na furaha huku akicheza kwa furaha na kuandika ujumbe wa kutupa vijembe kwa Kimambi akimuita kuwa mfitinishaji asiye na haya.
“Mwambie (PAPARAZI )pingamizi mwenye kiranga πππ SAMAKI KANASA KWENYE CHAMBOOOOOO,” Mama Dangote aliandika ujumbe huu ukidhaniwa kuwa mshale wenye sumu uliolengwa kwenye kambi ya Kimambi.
Awali, Kimambi alikuwa ameeneza uvumi kwamba Mama Dangote alikuwa amepata kiharusi na baada ya Mamake Diamond kujitokeza wazi, Kimambi naye alishikilia msimamo wake akisema kuwa alisema kiharusi hicho kilimkaba Mama Dangote Zaidi ya mwezi mmoja uliopita na kuonekana kwake pengine ameshapata nafuu.