Msanii Vanessa Mdee kutoka Tanzania ambaye kama miaka 4 hivi alihamia Marekani na kupata mpenzi kule amefichua kwamba tangu ahamie USA, si yeye wala wanawe wamewahi tia miguu yao katika malango ya maeneo ya kuabudu.
Mdee alifunguka ukweli huu wakati wa kipindi cha moja kwa moja kwenye Instagram yake na alisema kwamba imekuwa muda mrefu hajawahi kanyaga kanisani akiwa nchini Marekani.
Hata hivyo, Mdee alibainisha kwamba hiyo haina maana kwamba hajawahi fanya ibada ya kuabudu Mungu kwani huwa wakati mwingine wanafanya ibada ya nyumbani na familia yake.
“Hatujapata kanisa ambalo tunalipenda au kanisa la ukweli ambalo limejaa roho mtaktifu kwa hiyo hatuendi kanisani kama kanisani huku lakini mara kwa mara naingia kwenye streaming online, yeah,” Vanessa Mdee alisema.
Mdee baada ya kuchumbiana kwa Zaidi ya miaka 5 na msanii Juma Jux nchini Tanzania, penzi lao liligomba mwamba na mrembo huyo akaondoka zake Marekani ili kujaribu kutuliza moyo wake.
Akiwa Marekani ndiko alipatana na msanii ambaye pia ni mwigizaji, Rotimi mwenye asili ya Nigeria na wakachumbiana kabla ya kuoana.
Pamoja kwa kipindi cha miaka miwili, walifanikiwa kupata watoto wawili na kwa sasa wanaishi katika moja ya muunganiko wa kifamilia unaotajwa kuwa wa kupigiwa mfano.