Msanii anayejitapa kuwa bilionea kutokana na Sanaa, KRG the Don amejibu baada ya Wakenya wengi kumburuza mitandaoni wakimtaka kuiga mfano wa YouTuber wa Marekani, Mr Beast aliyewachimbia Wakenya visima 52 vya maji kimya kimya.
Wakenya mitandaoni walimtaka msanii huyo kutumia utajiri wake kwa kurudisha mkono katika maendeleo ya jamii ili kuonesha kama kweli yeye ni bilionea kama anavyojitapa.
Akijibu katika mahojiano na Mungai Eve, KRG alifoka vikali akisema kwamba licha ya kuwa tajiri bilionea, lakini haimaanishi kwamba anajukumika moja kwa moja kutumia pesa zake kwa miradi ya kuwanufaisha Wakenya.
“Mimi sina deni la Mkenya yeyote, mimi ni mwananchi tu wa Kenya, wewe mwenye unataka kusaidiwa tu, wewe umejisaidia aje? Mimi si Mungu na sina wakfu wowote. Mngojee Mr Beast awafanyie kazi,” KRG alisema.
Msanii huyo kwa tambo nyingi alisema kwamba Pesa zake si za kufanya kazi kama ambavyo bilionea huyo wa Marekani, akifichua kwamba hawezi kuwa na huruma na mtu ambaye hataki kujibidiisha kutafuta kazi akisubiri kusaidiwa.
“Pesa yangu ni yangu peke yangu, hata nisikie nilalie kama godoro ama nigawie watu wenye nataka, nasaidia yule mtu mwenye nataka. Mimi naweza nikakuangalia hapo uko na njaa na mimi nakula na hata shishtuki,” aliongeza.
KRG alitoa sababu ya kutokuwa na hulka ya kusaidia wafuasi na mashabiki wake.
“Sina deni la mtu, si hawa tu ni wale wale Wakenya wanashinda wakitusi wasanii hapa wakiomba msaada. Si ni ukweli? Tena ujisahau leo eti juu uko na kidogo uende uwasaidie, na ikiisha watakuchangia wewe ama wataanza kukuaibisha, lazima ufikirie hiyo kwanza,” alisema.
Wikendi kulikuwa na taarifa kwamba Mr Beast aliingia nchini kimya kimya miezi michache iliyopita na kuchimba visima 52 kwa jamii, kujenga daraja miongoni mwa miradi mingine ya kimaendeleo katika jamii.