Hatimaye msanii Harmonize ametua nchini Tanzania baada ya kuwepo nchini Marekani kwa siku kadhaa alikoenda kushuhudia kutolewa kwa tuzo za AEUSA 2023.
Msanii huyo aliweka historia kwa kushinda tuzo 3 kwa mpigo, na katika mahojiano yake ya waandishi wa habari pindi tu baada ya kutua katika uwanja wa ndege, alisema kuwa tuzo zake ni heshima na faraja kwa taifa kwani kupitia ushindi wake, taifa lilipata kuheshimiwa.
Harmonize alijibu kuhusu aliyekuwa babake katika kimuziki kumtambua na kumhongera kwa ushindi wa tuzo tatu.
Kwa mujibu wake, watu ambao wanaona tuzo hizo kuwa za kawaida hawajajitambua na kitendo cha Diamond Platnumz kumpongeza ina maana kwamba anajitambua.
“Ninachoweza kusema mimi ninajivunia uwepo wake [Diamond]. Hiyo ni dalili ya kujitambua, ukiona mtu anazungumza hivyo basi ujue amejitambua, kwa hiyo mimi najivunia. Na namshukuru sana,” alisema.
Diamond akizungumza katika hafla ya kumtambulisha msanii wake mpya WCB Wasafi, alimhongera Harmonize kwa kunyakua tuzo tatu katika hafla hiyo akisema kwamba siku zote furaha ya baba ni kumuona mwanawe akizidi kutusua kitaifa na kimataifa.
Diamond anachukuliwa kuwa baba wa Sanaa wa Harmonize kwani yeye ndiye aliyechangia umaarufu mkubwa wa msanii huyo baada ya kumchukua kutoka mitaani mwaka wa 2014 na baadae kuishia kumpa mkataba.
Hata hivyo baadae mambo yalienda songombingo baina ya wawili hao mwaka 2019 kupelekea kuvunja mkataba huo kwa njia ya kishari, jambo lililootesha uhasama mkubwa baina yao hadi leo hii.