Produsa mkongwe wa Bongo Fleva, Master Jay kwa mara nyingine ametia kwenye mizani tasnia ya muziki wa kizazi kipya baina ya Kenya na Tanzania.
Produsa huyo ambaye kwa sasa anajishughulisha na kutambua vipaji kupitia vuguvugu la Bongo Star Search nchini Tanzania alisema kwamba kuna tofauti kubwa baina ya muimbaji na mburudishaji – na wote wako kwenye tasnia ya muziki kama wanamuziki.
Jay aliweka wazi kwamba tofauti kubwa baina ya Kenya na Tanzania kimuziki ni kwamba waimbaji wazuri wanatoka Kenya lakini waburudishaji wazuri wanatoka Tanzania.
Pia alitambua kwamba Kenya imeizidi Tanzania katika matumizi ya lugha ya Kiingereza, jambo ambalo linawapa wasanii wa Kenya nafasi nzuri ya kutusua kimataifa kwa haraka kuliko wenzao wa Tanzania.
“Kitu ninachojivunia ni kwamba waburudishaji bora wa Afrika Mashariki wanatoka Tanzania, Wakenya wamebaki na kitu kimoja wanajua Kiingereza na wanatuzidi kuimba kuliko sisi, wana waimbaji bora sana,” Master Jay alisema.
Produsa huyo pia aliwakashfu wasanii wa Bongo kwa kusema kwamba jambo jingine ambalo linawazuia kutoboa katika soko la kimataifa ni kuiga midundo ya Magharibi na Kusini mwa Afrika badala ya kujitambua na mdundo wao wa kipekee kutoka Afrika Mashariki.
Alitolea mfano wasanii wa Nigeria wakubwa kimataifa na kusema kwamba wamefanikiwa kukwea ngazi hizo kwa sababu walikuwa na mdundo wao wa kipekee waliojitambulisha nao na kupendwa na mashabiki kutoka pembe zote za dunia.
“Tukitaka kwenda International lazima uwe na Identity yako, huwezi kuona Davido, Asake au msanii wa South Africa wanafanya sound ya BongoFleva. Kwa hapa East Africa wasanii wetu(Tanzania) ni bora na wanatengeneza pesa lakini hawatafika soko la kimataifa,” Master Jay alisema.