Siku ya Jumamosi, muigizaji tajika wa Kenya Catherine Kamau almaarufu Kate Actress alifurahi kukutana na Mkenya mwenzake anayefanya kazi katika duka la mvinyo jijini Dubai.
Kate ambaye amekuwa akifurahia likizo ya siku ya kuzaliwa katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati kwa siku kadhaa zilizopita alikutana na mhudumu huyo wa duka aliyejitambulisha kama Mwangi na wawili hao hata washiiki mazungumzo kwa lugha yao ya asili, Kikuyu.
Wawili hao walishiriki mazungumzo mafupi ambapo walisikika kufurahia jinsi watu kutoka jamii yao walivyosambaa kote ulimwenguni.
"Tuko kila mahali," Kate aliandika chini ya video ya mkutano wao ambayo alichapisha kwenye mtandao wa Instagram.
Mama huyo wa watoto wawili pia alifurahi kubaini kwamba mwanamume huyo aliyekutana naye na mchumba wake wa sasa wana jina sawa
“Tuko kila mahali, tunakuwanga kila mahali. Sasa, tutakuita aje?.. Mwangi, ata huyu (mpenzi wake) ni Mwangi ,” Kate alimwambia mhudumu huyo wa duka kwa furaha kubwa kabla yeye na mpenzi wake hawajaenda sehemu nyingine.
Kate, ambaye aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 37 mnamo Februari 3 yuko nchini Dubai pamoja na mpenzi wake wa sasa Michael Mwangi, ambaye amekuwa akiburudika naye katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.
Siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto wawili alishiriki video zake na Bw Mwangi wakiburudika na kujivinjari katika maeneo tofauti.
Katika moja ya video hizo, wapenzi hao wawili walionekana kwenye hoteli moja ya kifahari ambapo waliketi kwenye meza iliyojaa vitu tofauti vya kunywa na kula. Juu ya meza, pia kulikuwa na barua zenye jumbe za kheri ya siku ya kuzaliwa.
"Heri ya siku ya kuzaliwa Catherine. Nakutakia wakati mwema katika siku yako,” moja ya maelezo hayo yalisomeka.
Katika video nyingine, muigizaji huyo na mpenzi wake walionekana wakipanda gari pamoja kabla ya kuonekana kwenye sehemu ya burudani ambapo waliburudika na marafiki wengine.
Uhusiano mpya wa Muigizaji Kate Actress ulikuja kujulikana mwishoni mwa mwaka jana baada ya mama huyo wa watoto wawili kuanza kuonekana hadharani na mpenzi huyo wake mwenye ndevu nyingi. Haijabainika wawili hao wamekuwa wakichumbiana kwa muda gani lakini sasa ni wazi kuwa ni wapenzi.