Msanii pendwa wa midundo ya Ohangla, Evans Ochieng Owino maarufu kama Prince Indah ndiye rasmi msanii bora wa kiume kwa mwaka wa 2023.
Hii ni kwa mujibu wa Pulse Music Video Awards, tuzo ambazo hafla yake ilifanyika usiku wa Jumatano katika mgahawa wa Nairobi Street Kitchen.
Kwa mujibu wa jarida hilo la showbiz chini ya mwavuli wa shirika la Standard, tuzo za Pulse hulenga kuwatuza na kuwatambua wasanii wa Kenya ambao wanainua muziki wa Kenya kwa kiwango kipya kwa mkono mmoja.
“Muziki unabadilika kwa vizazi vingi, ukibadilika kutoka muziki wa kitamaduni hadi kwa Benga, Kapuka, Injili, Taarab, Reggae, Hip hop ya Kenya, na muziki wa Genge. Sasa, tuna Afropop, Afro-Fusion, Kenyan Rap (shrap), na Arbantone,” PMVA walisema wakipigia debe tuzo hizo.
Mwaka wa 2023 umekuwa wa kufana kwa msanii huyo wa Ohangla ambaye tungo zake na sauti yake vimekuwa vikiwavutia mashabiki wengi, wakiwemo wale ambao hawaelewi lugha ya Dholuo.
Miaka ya hivi karibuni, Indah alifanikisha kolabo zilizompa umaarufu nje ya jamii ya Dholuo, akifanya kolabo ya Adhiambo na Bahati kisha akarudi na ya pili ya msanii yuyo huyo na wakafanya Abebo – kisha akaja akafunga kazi na kolabo maarufu na msanii wa Mugithi, Samidoh – Bado Nakupenda.
Baada ya kutangazwa mshindi, Indah alijumuika kwenye jukwaa kuu kwa densi na watu maarufu akiwemo mkurugenzi mkuu wa MCSK Ezekiel Mutua ambaye alimtaja kama bingwa.
“Msanii maarufu wa Ohangla Evans Ochieng Owino almaarufu Prince Indah alishinda Msanii Bora wa Kiume wa Mwaka kwenye Tuzo za Video za Muziki za Pulse na akaamua kutuonyesha sababu! Hongera sana kaka. Wewe ni bingwa!” Mutua alimhongera.