Sasa ni wazi kuwa ndoa ya mwanasosholaiti Zari Hassan na mfanyibiashara Shakib Cham Lutaaya bado iko imara na Waganda hao wawili bado wako pamoja.
Wanandoa hao walithibitisha kurudiana kwao siku ya Jumatano waliposhiriki picha zao nzuri wakiwa pamoja kwenye sherehe za Umrah 2024 nchini Saudi Arabia.
Shakib alichapisha picha na video nzuri zake na mkewe kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuziambatanisha na jumbe za kupendeza na emoji za mapenzi.
"Chini ya kijani ni mahali ambapo nabii wetu mpendwa alizikwa," Shakib aliandika chini ya moja ya video alizochapisha.
Video na picha zingine ambazo kijana huyo wa miaka 32 alichapisha zilimuonyesha yeye na mkewe wakizunguka katika mji mzuri wa Riyadh nchini Saudi Arabia.
Zari pia alishiriki baadhi ya video na picha za ziara yao katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.
Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya ndoa ya Waganda hao kuripotiwa kusambaratika huku wote wawili wakishiriki jumbe za kimafumbo kudokeza wameachana.
Shida ilidaiwa kuanza baada ya video iliyomuonyesha Zari Hassan akitembea huku akiwa ameshikana mikono na aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Bosi huyo wa WCB alikuwa wa kwanza kuchapisha video hiyo kwenye ukurasa wake wa Instagram ambapo alimtambulisha mama huyo wa watoto wake wawili kama dada yake.
“Mimi na dada @zarithebosslady,” Diamond aliandika chini ya video hiyo.
Video hiyo iliyosambazwa wiki mbili zilizopita ilizua hisia mseto kutoka kwa wanamtandao tofauti ambao walitaka kuelewa kilichokuwa kikiendelea.
Zari alijibu, “aaai, nimekufa.”
Mume wa mwanasosholaiti huyo, Shakib alijibu kwa njia yake mwenyewe isiyo ya moja kwa moja ambapo alidokeza kwamba hakufurahishwa na maendeleo hayo.
"Watu wenye nia safi wapate watu safi wenye nia safi," alichapisha kwenye instastories zake.
Pia alishiriki, "Mitandao ya kijamii inakufanya uvutie watu ambao unapaswa kuwaombea."
Kijana huyo mwenye umri wa miaka 31 pia alifuta picha nyingi zinazomuonyesha akiwa na Zari kwenye ukurasa wake wa Instagram ikiwa ni pamoja na ile ya hivi punde aliyoshiriki mnamo siku ya wapendanao.
Zari hata hivyo alijibu madai ya Diamond kuvunja ndoa yake akidokeza kuwa mzazi mwenzake huyo si sababu ya migogoro ya ndoa yake.