Mama mzazi wa Zuchu, ambaye pia ni manii mkongwe wa Taarab kutoka visiwani Zanzibar, Khadija Kopa kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake kupigwa marufuku kwa mwanawe kutumbuiza katika visiwa hivyo.
Akizungumza kwenye Wasafi Media, Khadija Kopa alisema kwamba ishatokea ni kama ajali kazini lakini akafichua kwamba alishawahi kumuonya Zuchu kabla ya tukio hilo la kupigwa marufuku kwa kuimba matusi jukwaani.
“Ishatokea, ndio kama wanavyosema ajali kazini, ndio ishakuwa. Yataisha, hakuna jambo lisilokuwa na mwisho. Nimempa moyo lakini pia na mimi nimemwambia kuna vitu vingine…kabla hata haijatokezea yaani tuseme wakati mwingine mdomo wa mama unakuwa na nuksi Fulani. Mimi nilimwambia kama leo siku mbili tatu hivi marufuku hiyo ikaja kutokezea,” Khadija Kopa alifichua.
“Lakini ni vitu vya kawaida, ajali kazini. Nimemuelekeza kuwa na subira na utaendelea kuomba samahani na kila kitu kina mwisho wake,” aliongeza.
Zuchu alifungiwa kwa muda wa miezi 6 kutumbuiza katika visiwa vya Zanzibar kutokana na kupatikana na hatia ya kuimba matusi akiwa jukwaani.
Vile vile baraza la Sanaa Zanzibar, BASSF lilimpata na hatia ya kutumbuiza pasi na kuwa na kibali kutoka kwa baraza hilo, japo kuwa Zanzibar ndio nyumbani kwao.
Msanii huyo kando na marufuku ya miezi sita, pia alitakiwa kulipa faini ya shilingi milioni moja za kitanzania.