Kijana mmoja mwenye umri wa makamo katika ukurasa wa Instagram kwa jina Wisdom Igboke amewasimulia watu jinsi alifanikiwa kuwajengea wazazi wake jumba la kifahari baada ya kufanya kazi za aibu nchini Uingereza kwa miaka 4.
Igboke, raia wa Nigeria ambaye anafanya kazi jijini London, UK aliwakabidhi wazazi wake jumba la kifahari lenye vyumba 9 vya kulala wki tatu zilizopita na sasa amerudi kuwasimulia watu jinsi alifanikiwa kuwavuruta wazazi wake kutoka kwa lindi la umaskini.
“Mungu amenitumia kuwatoa wazazi wangu na familia kutoka katika umaskini. Jiunge name kusherehekea ninapowapa wazazi wangu maisonette ya vyumba 9 katika mji wangu wa nyumbani. Ndoto imetimia na ninamshukuru Mungu Mwenyezi. Kwa wale wote wanaohangaika kutaka familia zao zijivunie, Mungu akubariki pia na akutumie kuwafuta machozi familia yako. Hongera sana mimi na familia yangu,” Igboke aliandika wakati wa kukabidhi nyumba hiyo kwa wazazi.
Hata hivyo, baadae aliona watu wengi wameanza kumtupia maneno wengine wakimtaja kama aliyepata pesa za kujenga jumba hilo kwa njia za ulaghai.
Katika video ambayo alifanya kuelezea chanzo cha pesa zake kuwajengea wazazi nyumba, Igboke alisema kwamba wengi wanaongea tu kwa sababu hawakushuhudia mwanzoni mwa safari yake.
Kijana huyo alieleza jinsi alienda UK kujiendeleza kimasomo akiwa na pauni 100 peke yake, sawa ni elfu 16 za Kenya na baada ya kufilisika, akalazimika kufanya kazi zisizo rasmi, akisema hakuna hoteli jijini London ambayo haimjui kwa vile alikuwa anaoshea hoteli nyingi vyombo vya chakula kila siku ili kumudu maisha yake.
“Nilichapisha picha ya nyumba yetu na niliona komenti nyingi ambazo zilinifanya kushangaa shida ya watu ni nini. Watu walisema mambo mengi, wengine walisema mimi ni ‘wash wash’ lakini hawajui kwamba nimeosha sahani hotelini kwa miaka 4.” Alisema.
“Nilikuja UK miaka 4 kufanya digrii yangu ya Masters, mimi ni mtu ambaye ninawajibika sana, na pia ninajua jinsi ya kuweka akiba. Kwa mfano, mimi nimekuwa UK miaka 4 lakini bado sina gari, sio kwa sababu siwezi, lakini sababu najua gari huja na majukumu mengine.”
“Sasa hivi hakuna mtu anakumbuka nilichokipitia, mnaona tu mafanikio. Kwa taarifa yenu hakuna mgahawa Central London ambao haunijui, nilikuwa naosha vyombo wakati niliingia hii nchi mara ya kwanza nikiwa na pauni 100 pekee [Ksh 16,800]. Nilisimama Zaidi ya saa 11 kuosha vyombo, moto ukinochoma jikoni,” Igboke alisimulia.
Kando na kuosha vyombo, pia alisimulia jinsi alikuwa anawalea watu wazee, akisema aliosha miili ya watu wengi wazee kabla ya kumaliza masomo yake na sasa kupata kazi huko UK.