Mapema Jumatatu, Wakenya walirauka na taarifa za kusikitisha baada ya mafuriko makali kukumba eneo la Mai Mahiu kaunti ya Nakuru na kusomba makumi ya watu, na kuharibu mali yenye thamani isiyojulikana.
Inaarifiwa kwamba mafuriko hayo yalitokana na bwana moja eneo hilo kujaa na kuvunja kingo zake na kusomba vijiji.
Kufikia Jana, Zaidi ya watu 50 waliripotiwa kufariki na miili yao kuopolewa huku makumi ya wengine wakiwa bado hajawapatikana.
Katika moja ya tukio la kusikitisha ambalo limevutia hisia za huruma mitandaoni, ni baba mmoja ambaye alionekana akiubeba mwili wa mwanawe aliyeangamia wakati mafuriko hayo yalipobisha hodi.
Video hiyo ya kusikitisha ilionekana kumuathiri pakubwa msanii wa injili Kambua, ambaye ana historia ya kupoteza mwanawe mdogo pia.
Kambua kupitia ukurasa wake wa Instagram, alichapisha ujumbe wa kusikitisha akisema kwamba baada ya kuona video ile, alijihisi kutokuwa sawa kabisa, akisema kuwa taifa haliwezi kuwa sawa wakati maafa yanatokea kila kona.
“Niliona video ya mwanamume akiwa amebeba maiti ya mwanawe aliyeangamia kwenye mafuriko. Siko sawa kabisa. Hatuwezi kuwa sawa. Maafa mengi sana yanatuzunguka,” Kambua alisema kwa kusikitika.
Kambua amekuwa akizungumzia kwa ukakamavu jinsi amewapoteza wanawe wawili wachanga katika siku za nyuma.
Mwaka jana katika video ambayo alichapisha kwenye YouTube, Kambua alisema kwamba ilimchukua muda mwingi na ujasiri wa aina yake kuweka wazi jinsi amekuwa akipitia hali ngumu baada ya kuwapoteza wanawe katika nyakati tofauti.
"Wengi wenu mnajua kuwa nina watoto watatu, Nathaniel, Malaki mbinguni, na Natalie pamoja nami. Lakini ukweli ni kwamba nina watoto wanne. Hiki ni kitu ambacho sijawahi kushiriki na yeyote kati yenu hapo awali, lakini nadhani ni wakati wa kukuleta katika ulimwengu wangu na kukuambia kuhusu watoto wawili nilionao mbinguni na wawili ambao ninapata kuwatunza," alisema katika video hiyo.
Kambua hakufichua ni lini haswa alimpoteza mtoto wake mwingine lakini mnamo Februari 2021, mwimbaji huyo alitangaza kuwa amempoteza mwanawe mchanga, Malachi.