Mbunge wa eneo bunge la Mumias Mashariki Peter Salasya amefichua kwamba aliacha shule katika darasa la nne kwa miaka miwili na kufanya kazi katika viwanda vya sukari ili apate pesa kirahisi.
Wakati wa mahojiano Salasya alifichua kwamba ukaidi wake ndio uliomfanya kuacha shule kwa miaka miwili.
"Nilipokuwa nikikua, sikuwa na mambo mengi na ndiyo maana sikuwahi kuwa serious na maisha. Nilikuwa mkaidi sana na ndiyo maana nilipoanza shule sikuona umuhimu wa elimu. Niliamua kuweka shule kando darasa la nne na kwenda kufanya kazi katika viwanda vya sukari. ” Salasya alisema.
Salasya alisema maisha magumu ndiyo yaliyochangia uamuzi wake wa kuacha shule na kuongeza kuwa hakuwahi kufikiria kuwa angeweza kupanda ngazi ya kijamii jinsi alivyofanya.
Wakati wa mahojiano aliangazia kwanini amezama kwenye mitandao ya kijamii.
"Ninapenda mitandao ya kijamii, ilinipa jukwaa. Nakumbuka wakati nafanya kampeni sikuwa na mtu wa kusimamia jamii zangu. Nilikuwa meneja wangu mwenyewe, mwanablogu wangu. Saa ingine ningempa mtu simu yangu ili anirekodi wakati wa kampeni zangu.” Salasya alisema.
Hata hivyo alisema kuwa alikumbana na changamoto kwani alikuwa akiendesha shoo ya mtu mmoja na hivyo kuwa vigumu kwake kufanya kila kitu peke yake.
“Saa ingine nilikua napea mtu anirecord lakini kama ni mpinzani ukimaliza anadelete kila kitu. Lakini nikipata mzuri anihurumie ananichukua tu alafu naenda kwa club kwa free wifi naaza kuziedit nikizituma.” Aliongeza.