"Nililia sana leo!" Nazizi ataja mambo anayo'miss zaidi kumfanyia marehemu mwanawe

Amefichua jinsi alivyoangua kilio kwa kumkosa mwanaye akisema anatamani angalikuwa hai bado.

Muhtasari

•Nazizi alifunguka jinsi anavyomkumbuka mwanawe na kutaja mambo ambayo alikuwa akifanya na mvulana huyo na sasa hawezi kufanya.

•Haya yanajiri wiki chache tu baada ya rapa huyo mkongwe kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kifo cha mwanawe.

amezidi kumuomboleza mwanawe Jazeel Adam.
Nazizi amezidi kumuomboleza mwanawe Jazeel Adam.
Image: INSTAGRAM// NAZIZI HIRJI

Mwimbaji mkongwe wa Kenya Nazizi Hirji ameendelea kumuomboleza mwanawe Jazeel Adam, takriban miezi mitano tangu mvulana huyo wa miaka mitatu azikwe.

Jazeel, ambaye alikuwa mtoto wa pili wa rapa huyo alipoteza maisha mnamo Desemba 25, 2023 kufuatia ajali mbaya iliyotokea katika hoteli waliyokuwa wakiishi wakati wa ziara yao nchini Tanzania. Mwili wake ulirudishwa Kenya ambako alizikwa siku iliyofuata.

Katika taarifa yake Jumatatu jioni, Nazizi alifunguka kuhusu jinsi anavyomkumbuka sana mwanawe na kutaja mambo kadhaa ambayo alikuwa akifanya na mvulana huyo ambayo sasa hawezi kufanya kuona kwamba aliaga.

"Nataka tu kukushika, kukulaza, kukulisha, kukuogesha, kucheka na kukuchekesha, kucheza mpira na wewe na taf," Nazizi aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Aliongeza, ".. Kuenda matembezini, kujifunza lugha mpya ya ishara pamoja, busu mashavu yako .. lakini siwezi."

Mwanamuziki huyo mzaliwa wa Pwani aliendelea kufichua jinsi alivyoangua kilio kwa kumkosa mwanaye akisema anatamani angalikuwa hai bado.

“Nililia sana leo. Nakutaka tu hapa JAZ,” alisema.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya rapa huyo mkongwe kuonekana hadharani kwa mara ya kwanza baada ya kifo cha mwanawe.

Wiki jana, Nazizi aliandika ujumbe wa shukrani kwa watu wengi ambao wamempa sapoti katika kipindi cha zaidi ya miezi minne iliyopita wakati akimuomboleza mwanawe Jazeel Adams.

Mwimbaji huyo alichapisha video yake akiwashukuru watu wote ambao wamesimama naye, waliomtia moyo na kumuonyesha sapoti wakati akimuomboleza mwanawe.

“Habari zenu, najua sijakuwa hapa kwa muda. Lakini nataka tu kumshukuru kila mmoja wenu; mashabiki, familia na marafiki ambao wamekuwepo  kwa ajili yangu. Imekuwa safari chungu sana lakini nyie mmekuwa nami katika hayo yote na ninajaribu kurejea,” Nazizi alisema kwenye video hiyo aliyoichapisha kwenye Instagram.

Aliambatanisha video hiyo na taarifa nyingine ndefu iliyoandikwa kushukuru juhudi za familia, marafiki na mashabiki katika kumfariji.

"Nyinyi mmekuwa nguvu zangu, kila mtu kwenye DM zangu kwa miezi 5 iliyopita ninyi ni nguvu yangu. Kwa kila mtu ambaye ametembea nami kila hatua katika maumivu haya yasiyoweza kuvumilika. Ninawapenda nyote,” Nazizi aliandika.

Aliongeza, "Kwa ya wazazi kwenye DM  ambao wamepoteza watoto wakitoka kwenye maumivu yao ili kunitia moyo, ninahisi kushikamana na kila mmoja wenu kwa njia ambayo maneno hayawezi kuelezea. Nitatembea nanyi milele. Kwa wazazi wangu na Baba Jaz @therealtanaka asante kwa kuwa nguzo zangu uko imara!

Msanii huyo pia alimshukuru mtoto wake mkubwa Tafari Firaz ambaye alisema ameendelea kumtia moyo asihuzunike na kumkumbusha kuwa yuko na Mungu.

“Kwa marafiki zangu, dada zangu hasa!! Mnajijua wenyewe; Nimebarikiwa kuwa na mduara huu. Nawapenda. Sijawahi kupewa sapoti kiasi hiki maishani mwangu na hiyo ina maana kubwa kwangu katika wakati ambao ninahisi mateso kwa nafsi yangu, mnanikumbusha naweza kufanya hivyo,” alisema.