Gwiji wa reggea wa Jamaica, Gramps Morgan amuomboleza Jahmby Koikai kwa ujumbe mzuri

Gramps Morgan alimshukuru Jahmby kwa mambo makubwa aliyofanyia muziki wa reggae.

Muhtasari

•Gramps Morgan ameungana na maelfu ya wapenzi wa muziki wa reggae katika kumuomboleza marehemu Njambi Koikai.

•Lebo ya muziki ya CTBC Music Group ya Morgan Heritage, pia ilitoa heshima kwake kutokana na mchango wake mkubwa kwa muziki wa reggae.

amemuomboleza Jahmby Koikai
Gramps Morgan amemuomboleza Jahmby Koikai
Image: HISANI

 Mwimbaji Gramps Morgan, mmoja wa msanii wa bendi maarufu ya reggae kutoka Jamaica, Morgan Heritage, ameungana na maelfu ya wapenzi wa muziki wa reggae katika kumuomboleza marehemu Njambi Koikai.

Njambi ambaye alijulikana zaidi kama Fyah Mumma Jahmby alifariki dunia katika Hospitali ya Nairobi siku ya Jumatatu usiku  baada ya kuugua ugonjwa wa endometriosis kwa muda mrefu .

Huku akimuomboleza mtangazaji huyo wa reggae siku ya Jumatano, Gramps Morgan alimshukuru kwa mambo makubwa aliyofanyia muziki wa reggae. Aliomba roho yake ipumzike kwa amani na kubainisha kwamba watu hawatamsahau.

“PEPEA JUU KIPEPEO HATUTASAHAU 🇰🇪 ASANTE KWA YOTE ULIYOFANYA KWA MUZIKI WA REGGAE,UTAMADUNI NA WAKENYA WAZURI ❤️🙏🏾 PUMZIKA KWA AMANI MUMMA FYAAH,” Gramps Morgan alisema kupitia akaunti yake rasmi ya Twitter.

Lebo ya muziki ya CTBC Music Group, inayomilikiwa na bendi ya Morgan Heritage, pia ilimuomboleza Jahmby na kukiri heshima yake kutokana na mchango wake mkubwa katika muziki wa reggae.

Njambi ambaye alikuwa mpenzi mkubwa sana wa muziki wa reggea alipoteza maisha usiku wa Jumatatu, Juni 3 baada ya kuugua ugonjwa wa endometriosis kwa muda mrefu. Alikuwa amelazwa katika kitengo cha ICU cha hospitali ya  Nairobi alipofariki mwendo wa saa tatu usiku wa Jumatatu.

Marehemu ambaye alijizolea umaarufu wakati akitangaza vipindi vya muziki wa reggea kwenye redio na televisheni alikuwa ametatizika kwa takriban miongo miwili kutokana na ugonjwa wa endometriosis.

Wiki iliyopita, Jahmby alilazwa katika Hospitali ya  Nairobi na alituma ombi la damu aina ya  O positive.

"Habari familia, kwa sasa nimelazwa katika wadi ya pioneer ya hospitali ya Nairobi na ninahitaji Blood O positive. Tafadhali naomba wafadhili wa damu kwa Mary Njambi Koikai," posti iliyowekwa kwenye Instastori zake ilisoma. 

Mapema mwaka huu, mtangazaji huyo alisimulia safari yake na ugonjwa wa endometriosis.

Fyah Mummah alisema hali hiyo ilimfanya maisha yake ya ujana kuwa magumu. Aliifanya kazi yake kuwaelimisha watu juu ya ugonjwa huo.

Huku akionyesha picha yake ya zamani miaka sita iliyopita, Jahmby alinukuu,"Siku kama hii, miaka 6 iliyopita, nilifanyiwa upasuaji wa kubadilisha maisha kutokana na ugonjwa huu wa mwili mzima. Hatukuwa na habari kwamba ugonjwa huo ulikuwa umeathiri moyo wangu, mgongo wangu, appendix yangu (iliyotolewa), meno yangu; ufizi wangu, mapafu yangu, na diaphragm yangu, iligunduliwa kuwa na upungufu mkubwa wa damu.

Haikuwa hadi tulipofika kwenye Kituo cha Huduma ya Endometriosis huko Atlanta, tulipopata kujua jinsi ugonjwa huu ulivyokuwa umeenea na uharibifu uliosababishwa kwenye pafu langu la kulia na diaphragm baada ya makumi ya upasuaji.

Macho yangu yaliathiriwa na hivi majuzi ilibidi nipate dawa mpya. Nimehuzunishwa na miaka mingi iliyochukua kugundua ugonjwa huu.

Kutokana na ucheleweshaji huu, ugonjwa huenea karibu kila sehemu ya mwili. Kufikia wakati tunatafuta matibabu maalum, sasa tunapaswa kukabiliana na magonjwa mengine ya kinga ya mwili yanayosababishwa na Endometriosis na Adenomyosis."