Huddah kurejea Kenya kufungua kanisa lake, atangaza kazi kwa wahubiri na manabii chipukizi

Alitangaza atarejea Kenya baada ya takriban miaka miwili ambapo anapanga kuanzisha kanisa lake nchini.

Muhtasari

•Alifichua kanisa lake litajulikana kwa jina la ‘Huddah Ministries Prosperity Church’ na muziki wa kipekee utaimbwa na kuchezwa katika eneo hilo la ibada.

•Alidokeza kuwa ataunda nafasi za kazi kwani ataajiri wachungaji na manabii kadhaa chipukizi kuhudumu katika kanisa lake.

Huddah Monroe
Image: INSTAGRAM// HUDDAH MONROE

Mwanasosholaiti na mjasiriamali maarufu wa Kenya anayeishi Dubai, Huddah Monroe amefichua mpango wake wa kurejea katika nchi yake ya kuzaliwa.

Huddah amekuwa akiishi Dubai kwa miaka kadhaa iliyopita na huwa anarejea nchini mara kwa mara ili kuwajulia hali familia, marafiki na kuangalia mali yake.

Katika posti za Instagram alizochapisha siku ya Jumatano, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 32 alifichua kuwa atarejea Kenya baada ya takriban miaka miwili ambapo anapanga kuanzisha kanisa lake nchini.

“Wazo la kurejea Kenya kabisa kwa miaka miwili linanichosha sana kwa sababu niliuza gari langu nikifikiri sitaishi huko tena. Lakini kuna mradi wa Mungu ambao unanihitaji niwepo. Na vile Uber hizo ni Mwitu,” Huddah Monroe alitangaza kupitia Instastori.

"Kwa wale wanaoshangaa, ninarudi (Kenya) mnamo 2026, kufungua kanisa. Roho takatifu aliniita nifanye hivyo,” aliongeza.

Mjasiriamali huyo wa bidhaa za urembo aliendelea kufichua kuwa kanisa lake litajulikana kwa jina la ‘Huddah Ministries Prosperity Church’ na muziki wa kipekee utaimbwa na kuchezwa katika eneo hilo la ibada.

Pia alitangaza kwamba kila mtu atakaribishwa kanisani bila kujali dini yake.

“Waislamu pia wanakaribishwa katika Kanisa la Huddah Prosperity. Mahali panapokupa amani ya akili. Na hubadilisha maisha yako kutoka 0-100, "alisema.

Huddah pia alidokeza kuwa ataunda nafasi za kazi kwani ataajiri wachungaji na manabii kadhaa chipukizi kuhudumu katika kanisa lake.

“Kama wewe ni mchungaji au nabii mke chipukizi, nitaajiri. Shikilia Biblia yako na ujifunze,” alisema.

Aliongeza, “Kauli mbiu ya Kanisa la Huddah Properity; Kubadilisha maisha. Au inaweza kuwarudisha vijana kwa Mungu na mafundisho yake. Tutajadiliana.”

Mwanasholaiti huyo mrembo alidokeza kuhusu kuwahamasisha mashabiki wake wamsaidie kuchangisha pesa za kununua gari la kifahari ambalo atakuwa akitumia kuzuru nchi.