Staa wa Bongo, Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amefichua jinsi yeye na mpenzi wake Poshy Queen wanavyopanga kukwepa sehemu za umma ambapo watu wanaweza kumuona kwa urahisi.
Siku ya Alhamisi, bosi huyo wa Konde Music Worldwide alionyesha jengo ambalo linaendelea kujengwa ndani ya boma lake.
Alifichua kuwa jengo hilo litakuwa na chumba cha kufanyia mazoezi na saluni ya kibinafsi, akibainisha kuwa baada ya kukamilika, watu watalazimika kulipa pesa ili kumuona yeye na mpenzi wake.
"Gym yangu na saluni karibu kumalizika. Huwezi kuniona mimi na msichana wangu bure,” Harmonize alisema kwenye picha ya jengo linaloendelea kujengwa.
Kauli za Kondeboy zinaonyesha kuwa hatalazimika tena kwenda nje ya boma lake kwa ajili ya mazoezi au kukata nywele. Mpenzi wake Poshy Queen pia hatalazimika kwenda nje ya boma kutengeneza nywele zake.
Hatua hii inakuja wakati mapenzi ya mastaa hao wa Tanzania yakionekana kuendelea kunoga na uhusiano wao kuimarika.
Mwimbaji maarufu wa bongo fleva Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize ameendelea kukiri mapenzi yake mazito kwa mpenzi wake Poshy Queen huku uhusiano wao ukiendelea kuimarika.
Mwezi uliopita, Kondeboy alichapisha video iliyomuonyesha akimfuata nyuma mama huyo wa binti mmoja alipokuwa akienda chooni.
Chini ya video hiyo, alifichua kuwa kuandamana na mpenzi wake anapokwenda msalani sasa imekuwa jambo la kawaida kwake.
“Msichana mrembo zaidi niliyewahi kumuona duniani.. Kumsindikiza chooni ni swala la kawaida sasa!! Simuamini, sijiamini,” Harmonze aliandika chini ya video aliyochapisha kwenye mtandao wa Instagram.
Mastaa hao wawili sasa wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa miezi kadhaa iliyopita. Habari kuhusu uchumba wao ziliibuka mapema mwaka huu, na kusababisha mijadala mingi na msisimko kwenye mitandao ya kijamii.
Mnamo mwezi Machi, Poshy Queen alionyesha mapenzi yake kwa kumwandikia mpenziwe Harmonize ujumbe mtamu alipokuwa akifikisha miaka 30 leo.
Mwanasosholaiti huyo mrembo alitumia akaunti zake za mitandao ya kijamii kummiminia Konde Boy maneno matamu huku akitafakari hadithi yao ya mapenzi.
"Kwa mpenzi wangu na rafiki yangu wa karibu ❤️. Ninaomba kwamba miaka yako ya 30 iwe bora kwako na ufanikiwe kila kitu unachotaka, asante kwa kuniletea mimi na kila mtu karibu nawe furaha na furaha nyingi, NAKUPENDA SANA ADAMU WANGU ❤️.
"Kukuona ukiwa na furaha sana leo kunanifanya nijisikie mwenye furaha sana byb. Keep that smile on your face for me , God bless you for us daddy 🙏🏽. Happy birthday byb 😘," Poshy Queen aliandika.
Baada ya kuona ujumbe huo, bosi huyo wa Kondegang alijibu; "Kila kitu kwako mpenzi ❤❤❤❤❤ Asante nimebarikiwa kuwa na wewe ❤❤❤❤"