Inauma! Makokha abubujikwa machozi akikumbuka mazungumzo ya mwisho na marehemu mkewe

“Inauma, inauma! Ni uchungu kwa sababu sitakuwa tena na jiko yangu karibu ambayo nilikuwa naipenda,” alisema kwa uchungu

Muhtasari

•Muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alifichua kwamba yeye na mkewe walizungumza mara ya mwisho kuhusu ziara ya hospitali.

•Makokha alisema kuwa baada ya kufika nyumbani jioni hiyo, alikuwa na usiku mbaya kwani alilia sana hadi mida ya asubuhi.

amefichua mazungumzo ya mwisho na marehemu mkewe.
Makokha amefichua mazungumzo ya mwisho na marehemu mkewe.
Image: HISANI

Muigizaji na mchekeshaji mkongwe wa Kenya Mathias Keya almaarufu Alphonse Makokha amefunguka kuhusu mazungumzo yake ya mwisho na marehemu mke wakje, Purity Wambui.

Katika mahojiano na Tuko Kenya, muigizaji huyo wa Vioja Mahakamani alifichua kwamba yeye na mkewe walizungumza mara ya mwisho kuhusu ziara ya hospitali.

Makokha alifichua kuwa marehemu Wambui ambaye alikuwa akiugua wakati wa kifo chake alimuomba ampeleke hospitalini kutibiwa, jambo ambalo alifanya. Baadaye marehemu alitoa shukrani zake za dhati kwa mchekeshaji huyo mkongwe.

“Aliniambia ‘Daddy, nipeleke hosi’. Tukampeleka. Kufika huko akaanza kuhudumiwa. Akaniambia ‘Daddy, wewe ndiye bora’. Mungu wangu!” Makokha alisema huku akilia.

Muigizaji huyo mkongwe alifichua kuwa mkewe alifariki akiwa nyumbani. Alisema kuwa marehemu alikuwa chini ya uangalizi wa binti yao wakati alifariki.

“Nilikuwa naenda kazini. Nilikuwa nimewacha binti yangu nikamwambia amuangalie mama yake, naenda kutafuta riziki,” alisimulia.

Alifichua kuwa ni muigizaji mwenzake Hiram Mungai almaarufu Ondiek Nyuka Kwota ambaye alifahamishwa wa mara ya kwanza kuhusu kufariki kwa mkewe.

Ondiek kisha akamjulisha kuhusu habari hizo za kusikitisha kwa njia ya huruma.

“Nililia kwa muda wa saa mbili hivi. Mimi ndiye nilikuwa nikiendesha gari, yeye (Ondiek) alichukua usukani na kuendesha. Nikasema kwa sababu imefanyika, tuendelee na safari. Nikaenda kazini tu kama kawaida. Hiyo siku tulikuwa tulale lakini ata sikulala, lazima ningerudi. Mungu alinipatia nguvu nikawapeleka nyumbani vizuri, pia mimi nikafika nyumbani vizuri,” alisema.

Makokha alisema kuwa baada ya kufika nyumbani jioni hiyo, alikuwa na usiku mbaya kwani alilia sana hadi mida ya asubuhi.

Muigizaji huyo alisema tayari anakosa kelele ambazo mkewe alikuwa akimpigia nyumbani.

Alisema tukio hilo la kusikitisha limeacha jeraha kubwa ambalo hana uhakika kama litapona.

“Inauma, inauma. Ni uchungu kwa sababu sitakuwa tena na jiko yangu karibu ambayo nilikuwa naipenda,” alisema kwa uchungu mwingi.

Mke wa Makokha, marehemu Purity Wambui alipoteza maisha mnamo Juni 1, 2024 baada ya kuugua saratani ya matiti kwa muda mrefu.