Esther Musila asherehekea siku ya kuzaliwa ya 80 ya marehemu mamake kwa ujumbe maalum

Esther alisema kuzaliwa kwa mama yake kulikuwa kwa pekee sana kwa kuwa kuliwezesha pia yeye kuzaliwa.

Muhtasari

•Marehemu mama ya Esther ambaye alikufa takriban miaka nane iliyopita angekuwa akitimiza umri wa miaka 80 ikiwa bado angali hai.

•Aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri za kumbukumbu za marehemu mzazi huyo wake.

na marehemu mama yake.
Esther Musila na marehemu mama yake.
Image: INSTAGRAM

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za injili Guardian Angel, Esther Musila amesherehekea siku ya kuzaliwa ya marehemu mama yake.

Marehemu mama ya Esther ambaye alikufa takriban miaka nane iliyopita angekuwa akitimiza umri wa miaka 80 ikiwa bado angali hai.

Huku akiadhimisha siku hiyo maalum, Esther alisema kwamba kuzaliwa kwa mama yake kulikuwa kwa pekee sana kwa kuwa kuliwezesha pia yeye kuzaliwa.

“Leo ndiyo siku ya pekee zaidi mwakani kwa sababu kama si siku uliyozaliwa, mimi pia nisingalizaliwa,” Esther aliandika.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha nzuri za kumbukumbu za marehemu mzazi huyo wake.

Mke wa Guardian Angel alimsherehekea mwanamke huyo aliyemzaa akisema, "Wewe ndiye mtu mwenye  nguvu zaidi ambaye nimemjua maishani mwangu. Heri ya siku ya kuzaliwa ya 80 kwako mama  ukiwa mbinguni. Najua malaika wanasherehekea pamoja nawe. Tunakukumbuka.”

Mama huyo wa watoto watatu aliendelea kukiri kumpenda sana marehemu mama yake.

Mwezi Mei mwaka jana, mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 54  alimkumbuka marehemu mamake takriban miaka saba baada ya kuaga dunia.

Wakati akimsherehekea mzazi huyo wake, Bi Musila alimtaja marehemu kama nguzo kuu ya maisha yake.

"Ulinifundisha kuthamini kila siku ya maisha yangu na kuishi kana kwamba hakuna kesho. Nililelewa na mwanamke mwenye nguvu na najua kila wakati ulikuwa unasimama nami," alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Musila alimuombea mzazi huyo wake mapumziko ya amani na kueleza jinsi anavyojivunia miaka ambayo walishiriki pamoja.

Hata hivyo, alieleza anavyotamani marehemu angekuwa hai ili ashuhudie maendeleo yake na akutane na mumewe Guardian Angel.

"Mama, natamani ungeishi muda mrefu zaidi ili ukutane na mwanaume mzuri zaidi katika maisha yangu sasa. Najua ungefurahi sana kuniona katika nafasi hii mpya na najua tungekuwa tukiimba nyimbo uzipendazo pamoja," alisema.

Aliongeza,"Wajukuu zako pia wamefanya upate fahari kama vile ungetaka wafanye. Endelea kutuangalia sote hadi siku moja tutakapokutana tena. Tunakukumbuka na tunakupenda milele mama."

Musila alifichua kuwa mama yake alifariki akiwa usingizini, saa chache tu baada ya yeye na kaka yake kumtembelea.

Alitaja siku ambayo mamake alifariki kama siku ya giza zaidi maishani mwake huku akisimulia matukio yaliyofuata.

"Miaka 7 iliyopita, asubuhi kama hii, nilipokea simu kwamba mama yangu mpendwa amefariki usingizini. Hii ilikuwa chini ya saa 12 baada ya mimi na kaka yangu Fred kwenda kijijini kwa wikendi. Ilikuwa siku mbaya zaidi katika maisha yetu."  

"Bado sijui tulipataje nguvu ya kuendesha gari hadi Machakos, kwa kweli ilionekana kama ndoto. Ninaamini kabisa hadi leo kwamba Mwenyezi alilisuluhisha kwa njia yake mwenyewe na alitaka tutumie saa za mwisho za maisha ya mama pamoja naye," alisema.

Esther Musila alizaliwa Machakos yapata miaka 53 iliyopita na yeye ndiye mtoto wa kwanza kuzaliwa na binti pekee wa wazazi wake.