Rachel Ruto amsherehekea mume wake na babake kwa ujumbe maalum

Mke wa rais alimsherehekea baba yake na kumtambua kama mwamba na kielelezo chake.

Muhtasari

•Katika ujumbe alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Bi Ruto aliwapongeza akina baba wanaowajibika kwa uwepo wao.

•Huku akimsherehekea  Rais William Ruto, Rachel alimpongeza kwa furaha anayoiletea familia yao na kwa kujitolea kwake kwa ajili yao.

Image: TWITTER// RACHEL RUTO

Mke wa rais wa Kenya, Rachel Ruto, amemsherehekea mume wake William Ruto, baba yake na kina baba wengine huku dunia nzima inapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Akina Baba.

Katika ujumbe alioutoa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, Bi Ruto aliwapongeza akina baba wanaowajibika kwa uwepo wao.

Aliwapongeza akina baba na kuwaombea mema.

“Siku njema ya Akina Baba kwa akina baba wote katika taifa letu! Mmekuwa pale kwa ajili yetu katika hali ngumu na nyembamba; Mmetufundisha kuwa na nguvu na wema na kutokata tamaa kamwe. Mmetuonyesha maana ya kuwa shujaa wa kweli. Siku hii maalum na ijazwe na upendo, kicheko, na mambo yote yanayokuletea furaha. Mnastahili!,” Bi Rachel Ruto aliandika kwenye Twitter siku ya Jumapili.

Mke wa rais alimsherehekea baba yake na kumtambua kama mwamba na kielelezo chake.

"Kwa baba yangu, asante kwa kuwa mwamba wangu na mshauri wangu. Ninamshukuru Mungu kwa zawadi ya baba mkubwa,” aliandika.

Huku akimsherehekea mume wake, Rais William Ruto, Rachel alimpongeza kwa furaha anayoiletea familia yao na kwa kujitolea kwake kwa ajili yao.

“Kwa Bill wangu mpendwa, unaleta furaha na upendo mwingi katika maisha ya watoto wetu. Ninashukuru milele kwa kujitolea kwako kwa kila hatua ya njia kama baba. Heri ya Siku ya Akina Baba!” alisema.

Rachel aliambatanisha ujumbe wake kwa kina baba na picha nzuri inayomuonyesha akiwa na mume wake, rais William Ruto.