Bosi wa Kings Music, Alikiba amempongeza msanii mwenzake wa bongo fleva Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz katika hali ambayo imeonekana kuwa ya kushangaza.
Mwanzilishi huyo wa Crown Media amechukua hatua hiyo wakati akisherehekea jinsi muziki kutoka Tanzania ulivyokua na jinsi ulivyojizolea umaarufu kote duniani.
Akizungumza kwenye mahojiano ya hivi majuzi, Alikiba alitambua jinsi wimbo wa hivi punde wa Diamond, ‘Komasava’ ulivyotambuliwa na rapa wa Marekani, Chris Brown na kumpongeza kwa mafanikio hayo makubwa.
“Ni vizuri kuona msanii kama vile Diamond amefanya mpaka wasanii wa nje wanapenda kazi yake. Inamaanisha kwamba wanatusikiliza,” Alikiba alisema wakati wa mahojiano na Crown Media.
Aliongeza, “Sisi pia inatutia moyo kwamba muziki wetu unavuka mpaka unaenda sehemu mbalimbali na wanatusikiliza sana, kusema tu hawajapata vitu vimeweza kuwasisimua kama vile Komasava na ngoma zingine.”
Alikiba alibainisha kuwa wimbo wa Diamond kutambuliwa na msanii wa kimataifa ni msukumo kwa wasanii wengine wa Bongo.
Pia alikiri kutamani wimbo wake mmoja utambulike kama wa Diamond.
“Ata mimi ningetamani kuona msanii mwingine wa nje amecheza ngoma ya Alikiba . Inapendeza, vitu hatufanyi uchizi, hatufanyi vya kipumbavu, tunafanya kitu ambacho kila mtu anaweza akafurahia. Ni kitu kizuri, big up Diamond,” alisema Alikiba.
Hatua hiyo imeonekana kuwa ya kushangaza sana kwani mastaa hao wawili wa bongo fleva wanadaiwa kuwa wapinzani wakubwa zaidi katika tasnia ya muziki Tanzania.
Diamond Platnumz na Alikiba wamekuwa wakizozana kwa muda mrefu sasa na mastaa hao wawili wa bongo fleva katika siku za nyuma wamewahi kuonyesha wazi mara nyingi uhusiano mbaya kati yao.
Katikati mwa mwaka uliopita Diamond Platnumz alifichua kuwa anafanyia kazi mradi mpya wa muziki na kaka yake Alikiba, AbduKiba.
Diamond alitangaza hayo alipokuwa akizindua tamasha la Wasafi Festival ambalo aliwaalika bosi huyo wa Kings Music Records na mpinzani wake mwingine mkubwa Harmonize wa Konde Music Worldwide.
“Abdukiba (kaka yake Alikiba) atafanya collabo na mimi katika wimbo, nitakuwa naye kwenye tamasha na kaka yake Alikiba akiona inafaa, anaweza kuungana nasi, akitupa hata shoo moja tutashukuru. Harmonize pia, tunatakiwa kutumia akili zetu katika mambo haya, tusiweke mambo yetu binafsi kwenye haya mambo," alisema Diamond.
Huku akijibu mwaliko wa Diamond kwenye tamasha la Wasafi festival, Alikiba alibainisha kuwa hatakuwepo kwenye haflahiyo kwani atakuwa bize na mambo yake.
“Nipo bize na shughuli zangu,” alisema.