Mwimbaji maarufu wa nyimbo za Mugithi Lawrence Njugunga almaarufu DJ Fatxo ameweka wazi kwamba kuhusishwa na kifo cha marehemu Jeff Mwathi mapema mwaka jana hakukumuathiri kisaikolojia.
Katika mahojiano ya hivi majuzi kwenye Obinna TV, msanii huyo mwenye umri wa miaka 28 alisema kwamba anamshukuru Mungu kwani hakuishia kukumbwa na msongo wa mawazo kutokana na hali hiyo ngumu.
Hata hivyo alibainisha kuwa hali hiyo ilimvuruga akili kwani alianza kupokea chuki nyingi kutoka kwa wanamitandao, jambo ambalo hakuwa amelizoea.
"Namshukuru Mungu sikuweza (kukumbwa na msongo wa mawazo). Naapa kwa Mungu, ikiwa nilipatwa na huzuni, sidhani ningewahi pona,” DJ Fatxo alisema..
Aliongeza, “Jambo pekee lililokuwa ni kitu cha kukusumbua akili. Mimi nikiingia kwa usanii baada ya kuanza kuingia ngoma, mimi ni msanii ambaye naweza sema nilikuwa napendwa, yaani sikuwahi ona matusi yoyote kwa langu. Na mimi sikuwahi kuwa kwenye skendo yoyote. Mimi hadi sijawahi kushikwa na makarao, sijawahi kuwekwa pingu. Nadhani mahali nimetoka na shida tumepitia nyumbani hazituruhusu kuja nyumbani kuwa vijana wabaya na mambo mengine. Sisi tumezoea kujitafutia, tumezoea kuwa na bidi. Nimekuwa mtu mzuri na najua hilo.”
“Mimi nilishtuka sana kuona matusi kwa ukurasa wangu nikashangaa. Hiyo ndo kitu ilikuwa ngumu sana kupata nayo. Watu walikuwa wanatafuta damu yangu sana. Hizi maandamano tunafanya za kupinga muswada wa fedha, waliwahi kunifanyia sijui mara ngapi. Wanakuja tu wakisema ‘Mshikeni DJ Fatxo’. Lakini nashukuru Mungu sana kwa sababu yeye pekee ndiye alisimama nami.”
Huku akijitenga na kosa lolote katika kifo cha kijana huyo mwenye umri wa miaka 23, alibainisha kuwa yeye si mtu wa maana sana kuweza kukwepa haki.
Pia aliweka wazi kuwa maafisa wa uchunguzi hawakuona kosa lolote kwake na ndiyo maana hakuwahi kukamatwa hata siku moja.Alibainisha kuwa hakuna aliyeshtakiwa kuhusu kifo cha kutatanisha cha marehemu Jeff Mwathi.
Alieleza kuwa upande wa mashtaka haukuona sababu ya kufungua kesi kwa kuwa hakuna mtu aliyehusika katika tukio hilo, kama ilivyodaiwa na wengi.
“Hakukuwa na kesi. Kilichotokea ni kwamba, baada ya DCI kufanya uchunguzi, waliwasilisha faili lao kwa DPP kwa ajili ya kuchunguzwa zaidi. Ndipo DPP baadaye akagundua kuwa hakuna kesi. Kesi huwa inaundwa katika afisi ya DPP, kisha wanaipeleka kortini ili wajue kama kuna mtu anayepaswa kushtakiwa,” DJ Fatxo alisimulia.
Aliongeza zaidi, "Katika hali nzima, hakuna mtu aliyeshtakiwa kwa sababu hakuna mtu aliyefanya kile ambacho watu walikuwa wanasema. Nilikuja kugundua baadaye kuwa kinachotokea mtu anapojitoa uhai, faili halifungiwi katika kituo cha polisi. Inapelekwa mahakamani ili hakimu awasikilize ninyi nyote mnaofikishwa mahakamani kama mashahidi wa serikali.
Pamoja na DCI ambao ni mashahidi, mimi ambaye nilikuwa naye siku nzima, na mtu yeyote ambaye alitangamana naye au mtu yeyote ambaye aliona kitu cha aina hiyo. Ikifika pale, hakimu atasikiliza kila mtu na hatimaye ana mamlaka ya kufunga faili na kusema kuwa hajamkuta mtu yeyote mwenye hatia.”