Rapa Stevo Simple Boy kwa mara nyingine tena amechochea moto uliozima wa bifu yake na msanii anayejiita tajiri Zaidi nchini, KRG the Don.
Safari hii, Simple Boy ameamua kumtupia mkuki KRG kisa kuonyesha wazi msimamo wake wa kuunga mkono mswada wa fedha wa mwaka 2024, ambao ulikuja kutupiliwa mbali na rais Ruto baada ya kupitishwa bungeni.
KRG the Don alikuwa mmoja kati ya Wakenya wachache maarufu ambao walijitokeza kuonyesha kuunga mkono kupitishwa kwa mswada huo tata licha ya wenzake wengi kutoka tasnia ya burudani na Sanaa kusimama kidete kuupinga na hata kwa mara ya kwanza kuonekana barabarani wakijiunga na Wakenya walala hoi kuukataa mswada huo.
Stevo kwa maneno yake, alisema kwamba alihisi kabisa KRG aliwasaliti wenzake, kwani mswada huo pia ulikuwa na baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa na athari hasi kwa tasnia ya Sanaa.
“Jambo la kwanza ambalo ningependa kusema ni kwamba KRG ni rafiki yangu, lakini chenye alifanya si vizuri. Kwanza ametukosea sisi kama wasanii, angesimama na wasanii wenzake apinge mswada wa fedha. Jambo la pili pia yeye ni Mkenya, na ni mzalendo. Unaona sasa hiyo ni kama amesaliti nchi yake, unaona,” Simple Boy alisema.
“KRG chenye umefanya si poa, unafaa kwanza uombe msamaha kwa Wakenya na akaunti zako zitarudi. Unaweza weka video ya kuomba msamaha, su nenda kwa mahojiano omba msamaha na mwisho chagua kujitokeza kuungana na Gen Z na kuwaomba msamaha,” aliongeza.
Simple Boy pia aliradidi kwamba japo KRG anajiona amekuwa msanii mkubwa, bado hajamfikia yeye, akimkumbusha kwamba hata wasanii wakubwa kumliko walijitokeza kushiriki maandamano.
“Kwenye maandamano, hata wasanii wakubwa walijitokeza, kina Khaligraph na wengine. Sasa unaona kama wasanii wakubwa walienda, mbona KRG? Ndio ni mkubwa sijakataa lakini bado hajafikia kiwango changu. Katika moja hadi kumi mimi naweza kumpa tu alama 5, bado ako na safari ndefu sana kunifikia,” alisema Simple Boy.