Crazy Kennar apigwa na butwaa baada ya kutembelea hospitali ya Afrika Kusini kwa matibabu

Kennar amefichua kuwa hivi majuzi alitembelea hospitali moja nchini Afrika Kusini baada ya kuugua.

Muhtasari

•Msanii huyo mcheshi alifichua kuwa alipokea matibabu ya bila malipo katika hospitali ya umma, jambo ambalo lilimshangaza sana.

•“Nimeugua hapa SA leo, nilienda hospitali ya umma nashangaa nilitibiwa bure. Eeei, maajabu. Ingia ndani na utoke,” Crazy Kennar alisema.

Image: HISANI

Mtayarishaji wa maudhui na mchekeshaji wa Kenya Kennedy Odhiambo almaarufu Crazy Kennar amefichua kuwa hivi majuzi alitembelea hospitali moja nchini Afrika Kusini baada ya kuugua.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, msanii huyo mcheshi alifichua kuwa alipokea matibabu ya bila malipo katika hospitali ya umma, jambo ambalo lilimshangaza sana.

Alibainisha kuwa aliona ikiwa jambo la kushangaza kwamba wagonjwa wanaweza kutembelea hospitali na kwenda nyumbani bila kulipa chochote.

“Nimeugua hapa SA leo, nilienda hospitali ya umma nashangaa nilitibiwa bure. Eeei, maajabu. Ingia ndani na utoke,” Crazy Kennar alisema kupitia Instagram.

Huenda mtayarishaji huyo wa maudhui analinganisha sekta ya afya nchini Afrika Kusini na ile ya hapa nyumbani nchini Kenya. Nchini Kenya, watu hulipa kiasi fulani cha pesa kwa matibabu hata katika hospitali za umma.

Takriban miezi mitatu iliyopita, Kennar alithibitisha kwamba yuko nchini Afrika Kusini ambapo aliamua kujiunga na chuo kimoja kujiendeleza kimasomo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kennar alichapisha picha akiwa jijini Johannesburg kwenye ukuta wa chuo kimoja cha uchumi wa ubunifu na kusema kwamba ndio mwanzo ameianza safari mpya ya kiwango kingine cha burudani.

“Kiwango kipya cha burudani kimefunguliwa, safiri nami ninaposhiriki maisha yangu na wewe kama mbunifu wa Kienyeji wa Kenya anayesoma nchini Afrika Kusini,” Kennar aliandika kwenye picha hizo.

Mchekeshaji huyo aliweka wazi kwamba atakuwa anaishi Kenya na Afrika Kusini huku akifanya maudhui ya ucheshi duniani kote.

“Ninaishi nchini Kenya na Afrika Kusini huku nikitengeneza maudhui kote ulimwenguni,” Kennar alisema huku akimalizia kwa ahadi kwa mashabiki wake kwamba watarajie maudhui mengi ya uchekeshaji kibunifu kutoka kwake.

Safari ya Kennar kwenda kileleni ilianza akiwa bado chuoni.

Maudhui yake yalikua kwa kiasi kikubwa huku watumiaji wa mtandao wakiburudika na tabia yake katika ucheshi.

Kupitia maudhui yake, amekutana na watu kadhaa maarufu, akiwemo Trevor Noah ambaye picha yao ya pamoja ameisindika kwenye mwanzo wa picha zake Instagram.

Miezi michache iliyopita, mchekeshaji huyo alizua gumzo kwenye mtandao wa X baada ya kudai kwamba bado hajakabidhiwa maua yake na heshimu anayostahili kama mtu mbunifu Zaidi nchini Kenya kuwahi kuhishi.

Kennar alikwenda mbele na kutoa kidokezo kwa waandishi wa vitabu akiwaambia kwamba ni wakati sasa watunge mswada kumhusu, huku akiwapa mpaka mada ya mswada huo.