Wakenya walituma jumbe chanya kwa wanahabari wakubwa wa Royal Media Services Linus Kaikai, Yvonne Okwara na Mashirima Kapombe baada ya nambari zao za simu kufichuliwa mtandaoni.
Watu ambao hawakuwa na nia njema walifichua nambari za wanahabari hao watatu maarufu kwenye mitandao ya kijamii siku ya Alhamisi, na kuwataka watumiaji wa mitandao ‘wawasalimie’, neno ambalo linatumiwa kumaanisha ‘kuwanyanyasa kwa simu.’
Hata hivyo, idadi kubwa ya wanamtandao badala yake walitumia namba hizo kutuma jumbe nzuri kwa waandishi wa habari hao ambao walionyesha baadhi ya jumbe walizopokea.
“Siku gani! Nimefurahia kabisa kusikia kutoka kwenu nyote leo. Shukran sana kwa salamu!" Yvonne Okwara aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter.
Mwanahabari huyo mwenye sauti ya kuvutia aliendelea kuambatanisha ujumbe wake na screenshot za jumbe nzuri ambazo alipokea siku hiyo. Pia alidokeza kuwa alipokea mamia ya simu kutoka kwa Wakenya, ambao aliwashukuru sana kwa kumsalimia.
Mkurugenzi wa uhariri katika RMS, Linus Kaikai pia alifichua kwamba alipokea jumbe na simu nyingi kutoka kwa Wakenya baada ya namba yake kufichuliwa. Aliwashukuru wote ambao walimuonyesha upendo na kuwataka waendelee kuzungumza naye kwa njia nzuri.
“WAKENYA WENZANGU, nimefurahishwa sana na jumbe zenu nyingi za upendo, fadhili na kutia moyo. Hakika haya hayakuwa matokeo yaliyokusudiwa ya ‘mafupi’ hayo ya asubuhi na mapema. Asanteni kwa simu nyingi sana pia; Nilizungumza na watu wa ajabu sana. Wacha tuendelee kuzungumza, na kuipenda na kuitumikia Kenya 🇰🇪 kwa njia bora tuwezavyo. Mungu awabariki nyote,’ Kaikai aliandika.
Aliambatanisha ujumbe wake na screenshot za baadhi ya jumbe alizopokea.
Msomaji habari Mashirima Kapombe alibainisha kuwa waliofichua namba zao hawakutarajia kuwa wangetumiwa jumbe za upendo.
Aliwashukuru Wakenya kwa jumbe hizo nzuri na akaeleza matumaini yake kwa Kenya bora.
“Sidhani kama hivi ndivyo walivyotarajia... Asanteni kwa jumbe zote za fadhili na joto. Nyote mnanipa matumaini kwamba Kenya itashinda na tuko pamoja vizuri zaidi; anayejulikana na asiyejulikana, tajiri au maskini, Gen Z, Milenia, Gen X. Mungu akubariki ❤️ na nchi yetu kuu,” Mashirima aliandika.
Pia alionyesha baadhi ya jumbe alizopokea.