Siku moja baada ya mwimbaji wa injili kutoka Tanzania Bonny Mwaitege kuzushiwa kifo, msanii huyo amevunja kimya chake.
Kupitia video ambayo alirekodi akiwa kwenye studio ya kurekodi muziki, Mwaitege alisema kwamba alishangazwa na baadhi ya watu kumzushia taarifa za uongo kuwa amekufa hali ya kuwa yuko mzima na buheri kabisa wa afya.
Hata hivyo, alisema kuwa hii si mara ya kwanza kwake kuzushiwa taarifa za uongo kuwa ameufa na wala siye mwimbaji wa kwanza wa injili kufanyiwa dhuluma hiyo ya kisaikolojia.
“Nipo mzima kabisa wa afya kama mnavyoniona, sijapata matatizo yoyote, sijapata ajali yoyote, ni uzushi tu. Sijajua uzushi huu chanzo ni nini na ni nani ambaye anaanzisha uzushi huu mara kwa mara. Na sio kwangu tu peke yangu, ni waimbaji mbalimbali tumemsikia Bahati Bukuku, Rose Muhando, umesikia mimi hata sasa hivi ukiandika mitandaoni ‘mazishi ya Bonny Mwaitege’ utaletewa hadi jeneza, picha yangu na watu wakiniaga, sijui imekuaje?” alisema.
Mwaitege alisema kwamba uzushi huo sasa umemfika kwenye koo na amepata kushauriwa kuchukua hatua za kisheria ili kuwakabili watu vambao wamekuwa wakimuua angali hai.
“Nimekuwa nikipuuza lakini sasa nimepata ushauri na pia watu wameniambia kwamba ni vizuri nikajaribu kufuatilia jambo hili. Na naomba niwatoe hofu wapenzi na wafuatiliaji wa nyimbo zetu kwamba tayari nimelikabidhi jambo hili kwa watu ambao wana uzoefu, ni wataalamu na wapo kwa ajili ya hilo.”
Akizungumza kwa nini hakuwahi chukua hatua hapo awali alipozushiwa taarifa kama hizo juu ya kifo chake, Mwaitege alisema kwamba yeye ni mtumishi wa Mungu na hana muda mwingi wa kuvutana na watu, na ndio maana ameiachia serikali ili sheria ichukue mkondo wake.
“Pengine mtu anaamua tu anajua Mwaitege atanifanya nini? Ni kweli siwezi kufanya chochote kwa sababu kwanza mimi ni mtumishi wa Mungu na pili sina muda wa kuvutana na watu, lakini ninaamini Mungu atainua watu ambao watapambana kwa niaba ya sisi watumishi wa Mungu.”