Mwanamuziki Kelvin Bahati alikiri kuzidiwa na hisia baada ya kumtazama bintiye mzaliwa wa kwanza, Mueni Bahati, akionyesha talanta yake ya kuimba.
Shule ya Mueni ilikuwa imeandaa hafla ya kuonyesha vipaji siku ya Jumamosi na msichana huyo wa miaka minane ni miongoni mwa wanafunzi waliopanda jukwaani kuonyesha talanta zao.
Kwa usaidizi wa baadhi ya wanafunzi wenzake, alitumbuiza kwa ubora wimbo mmoja wa Bahati, ‘Lala Amka’, mbele ya hadhara ya wazazi, wanafunzi wenzake na wageni wengine waliokuwa wamekusanyika shuleni kwa ajili ya tukio hilo zuri.
“Jina langu ni Mueni Bahati, nataka kuwa mwimbaji nitakapokuwa mkubwa. Nataka kuwa msanii wa muziki. Lengo langu ni kuhamasisha, kubariki na kuponya watu. Ninataka kuwasilisha kwenu wimbo, kwa hivyo ketini chini, mpumzike na mfurahie,” Mueni alisema kabla ya kusema kuimba.
Malkia huyo mdogo aliendelea kutumbuiza vizuri kwa kujiamini na utulivu mwingi. Alipokaribia kumaliza kuimba, alielekea alipokuwa amekaa baba yake Bahati, akamshika mkono na kwenda naye jukwaani ili kuimba naye.
Katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa Instagram, Bahati alikiri kwamba kumtazama bintiye akitumbuiza jukwaani kulimfanya alemewe na hisia.
Alieleza fahari yake kwa bintiye na kumtakia heri.
“Leo nimelemewa na hisia 😍😍😍 Binti Yangu Amenishangaza kwa uchezaji wa muziki kwa Mara ya Kwanza Wakati wa Siku ya Talanta na Taaluma katika shule yao.. Najivunia kuitwa Baba yako @Mueni_Bahati ❤️❤️❤️,” Bahati alisema.
Jumamosi ilikuwa siku nzuri kwa Mueni Bahati huku wazazi wake wote wawili Bahati na Yvette Obura, wakijitokeza kumsapoti wakati wa hafla ya kuonyesha vipaji shuleni mwake.
Bahati alichapisha picha yake, bintiye Mueni na mwanawe Majesty Bahati wakiwa wamesimama kwenye uwanja wa shule.
"Ni siku ya talanta ya binti yangu Mueni Bahati shuleni kwa hivyo mimi na Majesty Bahati tulienda kumtazama akicheza," Bahati alisema chini ya picha hiyo.
Katika picha hiyo, watatu hao walionekana kuwa na furaha kwa kushiriki muda pamoja.
Kwa upande mwingine, Yvette Obura, ambaye ni mzazi mwenza wa Bahati aliposti video za binti yao akicheza mbele ya umati wa wazazi, wanafunzi na wageni wengine waliokuwa wamekusanyika shuleni.
Katika mojawapo ya video hizo, msichana huyo wa miaka minane alionekana akiimba wimbo wa babayake, ‘Lala Amka’, pamoja na watoto wengine huku umati ukishangilia. Huku akiendelea kutumbuiza, alienda mpaka alipokuwa amekaa Bahati, akamshika mkono na kumtaka asimame na kutumbuiza naye.
“Pigeni makofi basi.. tusimame basi,” Bahati alisema baada ya kukabidhiwa kipaza sauti na bintiye.
Yvette hakuweza kuficha furaha yake huku akimtazama bintiye akitumbuiza na mzazi mwenzake na alisikika akishangilia
Mfanyibiashara huyo pia alichapisha video nyingine iliyomuonyesha Bahati akitoa hotuba kwa wageni, na chini ya video hiyo, alimsherehekea mzazi mwenzake kwa kuwepo kwa ajili ya binti yao.
"Asante Baba Mueni kwa kuwa baba aliyepo na anayekusudia," Yvette aliandika.